Na Geofrey Stephen Arusha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amewataka Walimu kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wanafunzi na kuwafundisha kwa weledi mkubwa, ili kulisaidia taifa kupata Wataalam wakutosha katika nyanja za Uhandisi, Sayansi na Teknolojia.
Prof. Mdoe ametoa rai hiyo, wakati akifunga Mafunzo ya Walimu wa Sayansi na Hisabati mkoani Arusha, ambapo amesema serikali inahitaji kujenga na kuimarisha uchumi imara, na katika kutekeleza mradi wa SEQUIP, inatarajia matokeo chanya kutoka kwa walimu hao, baada ya kuwapatia mafunzo ya kuongeza ujuzi na umahiri katika ufundishaji na Ujifunzaji.
“Lengo la mafunzo kwenye mradi wetu ni kuongeza umahiri wa ufundishaji wa masomo haya, ili kuweza kutoa matokeo chanya, na huko tuendako kuna ushindani zaidi, tunahitaji Wanasayansi mahiri, wabunifu na ambao wanaweza kukabiliana na mabadiliko ya kidigitali katika ulimwengu wa sasa. Hatuwezi kujenga uchumi imara bila kuwa na Wanasayansi, maana hawa ndio wanaotusaidia katika sekta mbalimbali za kiuchumi, tusipokuwa na hawa watu tutapata wapi maendeleo, hivyo ni muhimu kuzingatia na kutekeleza kwa ukamilifu” alisema Prof. Mdoe.
Akizungumza kuhusu Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, amebainisha kuwa hayo ni Mapinduzi ya kidigitali, hivyo amewasisitiza Walimu kutumia fursa mbalimbali zitakazowawezesha kwenda sambamba na mabadiliko hayo, sanjari na kuwa na mtazamo chanya kutumia Tehema katika ufundishaji.
Ameeleza kuwa serikali kupitia mradi wa SEQUIP inatarajia kutekeleza ujenzi wa Shule mpya za Sekondari 1,000 katika kata ambazo hazina Shule na maeneo ambayo yana wanafunzi wengi ukilinganisha na miundombinu iliyopo.
“Kuanzia mwaka 2022/2023 serikali imejenga Shule mpya 232 kwenye kata zisizo na Shule za Sekondari nchi nzima. Pia fedha zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Shule nyingine 214. Wakati huo huo serikali inatarajia kujenga Shule mpya 26 za Sekondari za Kitaifa za Wasichana kila mkoa, ambapo ujenzi wa Shule 10 katika mikoa kumi upo hatua za umaliziaji na fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule 16 katika mikoa 16 zimeshatumwa kuanza ujenzi” amebainisha Prof. Mdoe
Ameongeza kuwa serikali imekamilisha upanuzi wa shule kongwe 18 na tayari imetuma fedha kwa ajili ya upanuzi wa shule nyingine 6.
Sanjari na utekelezaji wa shughuli hiyo, katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA, serikali imetoa vifaa pamoja na kutenga fedha shilingi bilioni 6 kwa ajili ya kununua vifaa hivyo kwa Shule 500 za Sekondari.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) Dkt. Meigaru Mollel amesema walimu 1,204 wa Sayansi na Hisabati wamepatiwa mafunzo, ambapo 317 ni walimu wa Bailojia, 312 Fizikia, 324 Hesabu na 250 walimu wa Kemia.
Mwenyekiti wa Wawezeshaji wa Mafunzo hayo Dkt. Emmanuel Sulungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kuona umuhimu wa kuboresha miundombinu ya Elimu Nchini pamoja na kujali mahitaji ya walimu kwa kuwapatia mafunzo endelevu kazini, huku akiwataka walimu hao kutekeleza kwa umahiri wa hali ya juu ili kupata matokeo chanya kulingana na thamani ya uwekezaji katika mradi huo.
Mwisho .