Na Geofrey Stephen Arusha .
Naibu Katibu Mkuu wizara ya Mifugo,Dokta Daniel Mushi ameutaka uongozi wa wilaya ya Longido kujipanga na kuweka doria za kutosha mipakani ili kuzuia utoroshaji wa mifugo ambayo inapelekwa nchi jirani ya Kenya na kupelekea kuwepo kwa upungufu wa mifugo nchini.
Ameyasema hayo leo agosti 30 ,jijini Arusha akiwa katika ziara yake ambapo ametembelea mnada wa Mifugo katika eneo la Meserani pamoja na kiwanda cha kuchakata nyama cha Elia food Overseas kilichopo wilayani Longido mkoani Arusha. .
Dk Mushi amesema , kumekuwepo na uhaba mkubwa wa Mifugo hapa nchini hivi sasa changamoto inayopelekea kushuka kwa soko la Mifugo kutokana na utoroshaji wa Mifugo hiyo kwenda nje ya nchi jambo ambalo linaikosesha serikali hasara kwani haipati mapato yoyote.
“Jamani katika hili nawaagiza viongozi wote wa wilaya ya Longido mkae pamoja na kuunda timu maalumu ya kufanya doria katika maeneo ya mipakani ili kudhibiti utoroshaji huo ambao unafanywa na wafugaji kwa lengo la kutafuta soko nje ya nchi kwa njia zisizo halali jambo ambalo linaikosesha serikali mapato yake na kuendelea kupungua kwa Mifugo hapa nchini. “amesema Dk Mushi.
Amewataka viongozi hao pia kukaa na Wazee wa kimila (Malwaigwanan) ili kuweza kuwaelimisha watoe elimu kwa jamii zao za wafugaji kuhusu madhara ya utoroshaji kwani Mifugo inapotoroshwa serikali ndo inapata hasara kubwa.
“Moja ya changamoto iliyoelezwa kuchangia kuwepo kwa utoroshaji ni ukosefu wa maji kwa ajili ya kulishia malisho hayo ,sisi kama serikali tutaangalia namna ya kujenga mabwawa ya kutosha na naombeni halmashauri pamoja na wawekezaji waangalie namna ya kujenga mabwawa ya kutosha ili mifugo isitoroke nchi jirani. “amesema.
Aidha amewataka wawekezaji kuboresha bei zao wanazonunulia Mifugo hapa nchini ikilinganishwa na nchi jirani kitendo kinachopelekea mifugo mingi kukimbilia huko,hivyo kuwataka kuboresha bei zao ili wafugaji wauze mifugo yao hapa nchini na kuondokana na uhaba huo.
Kwa upande wa Wakurugenzi wa kiwanda cha Eliya food Overseas Ltd ,Shabbir Virjee na Irfhan Virjee wamesema kuwa,hivi sasa wamepunguza uzalishaji kiwandani kutokana na upungufu wa Mifugo ambayo nyingi inapelekwa nchi jirani na hivyo kupelekea wao kukosa soko hilo na hivyo kuishia kupata hasara kubwa.
Irfhan amesema ,kipindi cha nyuma walikuwa wanachakata mbuzi na kondoo elfu nne kwa siku ambayo ni sawa na tani hamsini kwa siku ambapo baada ya kupata changamoto ya ukosefu wa Mifugo kuanzia mwezi sita na kufanya uzalishaji kushuka na kufikia mbuzi na kondoo mia tano kwa siku kutokana na Mifugo hiyo kuuzwa nje ya nchi.
Aidha amesema kuwa, kutokana na changamoto hiyo imepelekea kukosa soko la nje walipokuwa wameingia nao mkataba kwa ajili ya kuwapelekea nyama hali ambayo inawapelekea kutafuta Mifugo ndani na nje ya nchi ili kuendelea kulinda soko hilo ambalo tayari wana mkataba nao wa kuhakikisha wanapeleka nyama ya kutosha.
Nao baadhi ya wafugaji wakizungumzia changamoto hiyo waliomba serikali kuwaboreshea mazingira mazuri kwa wawekezaji hapa nchini ili waweze kuuza bei nzuri kama ambavyo nchi jirani ya Kenya inafanya kununua mifugo kilo shs 14,000 tofauti na hapa nchini ambapo wananunua kwa kilo shs 9,300 kwani kuna tofauti kubwa sana ya bei ,jambo linalopelekea wafugaji wengi kukimbilia nchi jirani ya Kenya.
Mwisho.