Site icon A24TV News

SERIKALI YATENGA BILIONI 9 KUKUZA UJUZI KWA VIJANA KILA MWAKA

Geofrey Stephen Arusha

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu kazi,vijana,Ajira na wenye Ulemavu Prof Joyce Ndalichako amesema Serikali hutenga kiasi Cha Bilioni 9 kila mwaka kwa ajili ya kukuza ujuzi kwa vijana katika program maalumu ya Taifa ya kutoa Mafunzo ya uanagenzi na kukuza ujuzi kwa waliopo  Kazini.

Akizungumza  mkoani Arusha kwa niaba ya Waziri Ndalichako Mkurugenzi  msaidizi Ofisi ya Waziri mkuu anayeshughulikia ukuzaji wa ujuzi Robert Masingiri  wakati alipotembelea mradi huo unaotekelezwa katika Chuo Cha Taifa Cha Utalii  tawi la Arusha alisema vijana zaidi ya 130000 wamenufaika na programu hiyo.

“Program hii ilianza mwaka 2016 baada ya Serikali kukaa pamoja na waajiri wakakubaliana kuwa ni lazima kuwe na program ya nchi ambayo itahusika  kukuza ujuzi kwa vijana ili waweze kujiajiri na kuajiriwa, na Ina maeneo makuu manne ambayo ni mafunzo Kwa njia ya vitendo,kurasimisha ujuzi mahali pa kazi, mafunzo ya utarajali(internship) na eneo lingine kukuza ujuzi kwa waliopo Kazini kulingana na  mabadiliko ya teknolojia” alisema Masingiri.

Aidha alisema kwa mwaka huu wa Fedha 2023/2024  tayari Serikali ilishatenga sh. Bilioni 9  ambapo mwezi  Julai kiasi cha sh. Bilioni 5 zilishatolewa  kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

“Ni wakati wa vyuo  vyenye Sifa husika kuchamgamkia fursa ya kupeleka Maombi wizarani ili kusudi kuanza utaratibu wa kudahili vijana kwa ajili ya program hii na mwisho wa kupeleka Maombi  ni mwezi huu na ifikapo oktoba mwaka huu tunatarajia kuona vijana wanajiunga  kwa lengo la kupata fursa hizi” alisema.

Naye mkuu wa Chuo hicho Dk. Florian Mtei  alitumia fursa hiyo kuishukuru Ofisi ya Waziri mkuu kuendelea kutoa fursa hiyo Kwa vijana ambapo aliwaasa vijana kuitumia vizuri fursa hiyo kwa  malengo ili kupata ujuzi.

Akieleza moja ya matatizo yaliopo katika utekelezaji wa program hiyo alisema ni pamoja na vijana kushindwa kumudu gharama za maisha ikiwamo chakula na malazi pindi wawapo chuoni huku akieleza kuwa pamoja na ada kutolewa lakini wapo vijana wanaoshindwa njiani kuendelea na  mafunzo  hayo kutokana na kushindwa kujikimu kimaisha.

“Tunafahamu nia ya Serikali kuwa ni njema katika kuwasaidia vijana lakini ningeomba kile kinachotolewa kwa kila kijana angalau kiongezwe kidogo kama Kuna uwezekano Kwa lengo la kuwasaidia vijana waweze kumudu gharama za maisha kutokana  na wengi kushindwa njiani kwa kushindwa kumudu maisha ikiwemo chakula na malazi” alisema Mtei.

Aliiomba Serikali pia kutoa wigo mpana  kwa vyuo husika kufanya udahili peke yao ili kufahamu aina ya vijana wanaowachukua Kwa lengo la kuwasaidia zaidi kulingana na uwezo walio nao huku akidai kuwa endapo watafanyiwa udahili na watu tofauti na wakufunzi inakuwa ngumu kuwapanga katika mafunzo husika kulingana na uhitaji au uwezo wa kijana.

Mshiriki wa programu hiyo Joseph Joseph katika fani ya uongozaji utalii aliiomba Serikali  kuwasaidia kama kuna uwezekano wa kuwasemea ili  wale wenye nia ya kujiendeleza kwa  kozi ya Muda mrefu baada ya mafunzo hayo wapunguziwe ada Kwa ajili ya kupata ngazi ya astashahada(cheti) na Stashahada (Diploma)  waweze kuwa na ujuzi kamili.

Naye mnufaika  mwingine Jackline Rite aliiomba Serikali kuwapatia mkopo pindi wanapomaliza kozi hizo Ili waweze kujiajiri wenyewe ambapo alisema kupata ujuzi ni hatua moja lakini ujuzi bila mtaji bado tatizo linabaki pale pale, sambamba na kuomba kuongezewa  muda wa kujifunza mafunzo hayo Ili kupata muda mwingi wa kufanya vitendo zaidi.
Mwisho.