Matukio ya uhalifu ,ubakaji na wizi yazidi kutikisa kata ya Daraja mbili mkoani Arusha .
Na Geofrey Stephen Arusha .
Matukio ya uhalifu katika kata ya Daraja Mbili Mkoani Arusha yamezidi kushika kasi mara baada ya Mtendaji wa kata hiyo John Joseph kunusurika kuchomwa kisu cha ubavuni na kibaka wakati akiwa katika harakati za kumwokoa msichana aliyetambulika kwa jina la Caren Nyangasa (20) aliyenusurika kufanyiwa kitendo cha ubakaji na kibaka aliyetambulika kwa jina la Bolo young .
Akizungumzia tukio hilo,Mtendaji wa kata hiyo amesema toka mei mwaka huu hadi sasa hivi kata yake imekuwa na matukio makubwa ya uvunjifu wa amani ikiwemo wananchi kuvunjiwa nyumba zao wanawake kufanyiwa vitendo vya ubakaji pamoja na wizi wa kuibiwa vifaa vyao vya dhamani ndani ya nyumba zao .
“Mimi baada ya kusikia kelele hizo niliwahi eneo la tukio kwani nilikuwa karibu na nilipofika huyu kijana alichomoa kisu akataka kunipiga cha ubavuni lakini nashukuru Mungu watu waliwahi kuniokoa ndipo huyo kijana alipokimbia na wananchi hawakufanikiwa kumkamata kabisa.”amesema John Mtendaji huyo.
Wakizungumzia Tukio hilo,Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kijana huyo Bolo young ni miongoni mwa majambazi sugu walionusurika kifo mara baada ya mwenzao mmoja kuchomwa moto na kufariki dunia hivi karibu aliyetambulika kwa jina moja la Ludo .
Ambapo wamesema kuwa, kijana huyo anazidi kuleta hofu kubwa kwa wananchi wa kata hiyo kwani wanajikuta wanaishi kwa wasiwasi sana kutoka na kushamiri kwa matukio iwe usiku na mchana jambo ambalo wameomba jeshi la polisi kuliangalia kwa jicho la pili kwani linahatarisha maisha yao.
Kwa upande wake Caren akielezea tukio hilo amesema alitoka nyumbani kwenda kufanya huduma ya kutoa pesa katika simu yake ndipo “Bolo young” kumkamata na kumziba mdomo na kumkaba na kuanza kumvua nguo akitaka kufanya naye mapenzi kwa nguvu ndipo akapiga kelele ambapo wananchi walijitokeza wakampa msaada na ndipo Bolo young kukimbia kusipo julikana .
“Kwa kweli kitendo hiki kimeniogopesha sana kwani kama sio kupiga kelele huyu kibaka angenibaka maana alishaanza kunivua nguo huku akiniziba mdogo ili nisipige kelele ila namshukuru Mungu na hata wananchi waliowahi kuniokoa kwa kweli jambo hili limenipa uoga mkubwa sana.”amesema.
Amesema matukio ya ubakaji katika kata hiyo kwa sasa ni changamoto kubwa sana mara baada ya kuwepo kwa wimbi la vijana wanaojiita tatu mzuka kuunda genge la ujambazi na kubaka katika kata yao ya daraja mbili.
Naye Mama Mwenye nyumba aliyejitambulisha kwa majina ya Rose Stanley anapoishi Caren amesema ni kweli alisikia kelele nje ya nyumba yake na baadaye kutoka nje kutazama na kukuta mpangaji wake Caren amelazwa chini na kijana akitaka kumbaka kwa nguvu akisema ataua mtu au yeye auawe .
“Kitendo hiki kilichofanywa na kijana huyu ni kitendo cha kinyama sana kwani kinahatarisha maisha yetu kwani amekuwa tishio kubwa katika kata ya daraja mbili na kuwafanya wananchi waishi kwa wasiwasi mkubwa sana .”amesema .
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Prosper Msofe akizungumzia tukio hilo amesema kata yake kwa sasa imekuwa miongoni mwa kata korofi ambazo jeshi la polisi mkoani Arusha linahitaji nguvu ya ziada kwani mpaka sasa vibaka wamekuwa sehemu ya kuweka kambi na kufanya uhalifu mkubwa kwa wananchi wake.
Msofe amesema jeshi la polisi mkoani Arusha limekuwa mwiba kwake kwa kitendo cha yeye kupiga simu kwa kamanda wa polisi mkoa wa Arusha bila kupokelewa mara kadhaa jambo ambalo linamweka katika wakati mgumu sana .
Msofe amesema tukio la mtendaji wa kata kunusurika kuchomwa kisu sio la mara ya kwanza bali ni matukio ya mara kwa mara huku akipeleka kilio chake kwa mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP kuingilia kati kwani polisi mkoani Arusha hawampatii ushirikiano wowote kwa ajili ya usalama wa wananchi wake .
“Kata yangu imekuwa genge la wahuni wabakaji wezi ambao ni majambazi sugu naomba viongozi wa chama cha Mapinduzi Ccm wanisaidie kwani nimekuwa kiongozi wa kuongoza wananchi walemavu wanaokatwa viungo vyao kila kukicha na vibaka hao na mimi naonekana sina msaada wowote kwa wananchi wangu wakati najitahidi kupambana usiku na mchana .”amesema Msofe
Kwa upande wa Balozi wa nyumba kumi wa mtaaa wa jamhuri Zubira Saidi amesema kitendo cha Mtendaji kunusurika kuchomwa kisu sio la kufumbia macho kwani mtaa wake na kata kwa ujumla una changamoto ya matukio makubwa ya uvunjifu wa amani kwa viongozi na hata wananchi wake pia.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Felician Mtahengerwa baada ya kupigiwa simu na diwani wa kata hiyo alituma polisi kufika eneo la tukio ambapo walifanikiwa kukamata watuhumiwa 4 huku mhusika wa tukio hilo akiendelea kusakwa pamoja na watuhumiwa wengine .
Mwisho.