Site icon A24TV News

MKURUGENZI BAGAMOYO ATAOA UFAFANUZI JUU YA KUVUJA MTIHANI DARASA LA SABA

Na mwandishi wetu

Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Bagamoyo Mkoani Pwani Shauri Selenda amewatoa hofu Watanzania juu ya taarifa zilizosambaa kuhusu njama za kuvuja kwa mtihani wa taifa wa darasa la saba unaotarajiwa kufanyika wiki hii kote nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Selenda alisema amepokea taarifa za baadhi ya maafisa wake kuhusishwa na hujuma na wizi wa mtihani wa mwaka 2023 katika shule ya awali na msingi ya Baobao na tayari amechukua hatua za kuwaengeua katika zoezi la usimamizi wa mitihani hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na kutajwa kwenye tuhuma hizo.

“Taarifa hizi zimetufikia na tayari tumeanza kuzifanyia kazi kwa kuwaweka pembeni katika suala zima la usimamizi wa mitihani na tumeunda timu ya uchunguzi kama wilaya tuone kama waliotajwa wanahusika ili hatua za kisheria zichukuliwe”. Alisema Selenda.

Na kuongeza kuwa “Kutokana na tuhuma hizi kama wilaya tumeimarisha ulinzi katika vituo vyote vya kufanyia mitihani, hivyo napenda kuwatoa hofu wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu suala hilo”.

Alisema taarifa hiyo inaonyesha kuwa mbali ya waliotajwa kunamtandao mkubwa unaohusisha watu wengi kuanzia Baraza la Mitihani la Taifa hadi Wizara ya Elimu, hivyo uchunguzi huo utaendelea kwa ngazi zote.

Akizungumza kwa njia ya simu ya kiganjani afisa uhusiano wa Balaza la Mitihani la Taifa John Nchimbi alisema taarifa hizo wamezipokea na kuahidi kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo.

“Ndugu wandishi wa habari taarifa hizi tumezipokea na tutazifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili tubaini ukweli wa jambo hilo, ikibainika kila aliyehusika atachukuliwa hatua za kisheria”. Alisema Nchimbi.

Taarifa iliyotumwa kwa Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda inaonesha imeandikwa na baadhi ya walimu wanaojiita wazalendo katika shule ya Baobab iliyopo Wilayani Bagamoyo imewataja waliohusika na njama hizo kuwa ni Mratibu wa Elimu Kata ya Mapinga Franco Zemba, Afisa Elimu taaluma Wilaya ya Bagamoyo Estar Lumato na vigogo kutoka Baraza la Mitihani la Taifa.

“Mh. Waziri, mwenzetu mmoja alishiriki hujuma mwaka jana, mwaka huu ameshiriki tena katika kikao cha kukamilisha mikakati ya hujuma ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2023, baina ya Mwalimu Mkuu wetu na mratibu wa Elimu Kata ya Mapinga Franco Zemba. Kikao hicho kilifanyika Agosti 28 2023”. Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Alipotafutwa Meneja wa Shule ya Baobab Amina Nyange ili kutolea ufafanuzi juu ya tuhuma hizo zinazoikabili shule yake alisema kuwa suala hilo halipo na halijawahi kuwepo na wala hawana mpango wa kufanya hivyo.

“Hilo linalosemwa kwetu halipo na halijawahi kuwepo na wala hatuna huo mpango wa kufanya hivyo, peleka panapohusika ili wafanye uchunguzi wao na kubaini ukweli”. Alisema Nyange.