Site icon A24TV News

MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamia ujenzi wa barabara kutunza mazingira

Na Mwandishi wa A24tv

MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka amesema baraza hilo litahakikisha linasimamia kwa ukaribu ujenzi wa Barabara ya Katumba-Lupaso wilayani Rungwe yenye urefu wa Kilomita 35 ili kuhakikisha hauathiri mazingira.

Dkt. Gwamaka ameyasema hayo alipoambatana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) pamoja na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) kwenye uzinduzi wa Barabara hiyo ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami.

Amesema Barabara hiyo inapita kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na mito inayotiririsha maji yake kuelekea Ziwa Nyasa na hivyo ni lazima wahakikishe ujenzi wake hauathiri vyanzo hivyo ambavyo ni muhimu kwa ustawi wa binadamu na viumbe wengine.

“Miradi kama hii ya barabara huwa inafanyiwa tathmini ya athari kwa Mazingira na kwa maeneo hasa ya mito tunakuwa makini zaidi kuona hapaathiriki na ujenzi wa barabara, Tutashirikiana na wenzetu wa Bonde la Ziwa Nyasa kulinda vyanzo hivyo, tusipovilinda vitakauka na hata ziwa letu litakauka na hivyo kusababisha kukosekana kwa maji, kwahiyo sisi kama wasimamizi wa mazingira tutahakikisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 inafuatwa,” amesema Dkt. Gwamaka.

Vilevile amesema maeneo mengi ambayo Barabara hiyo inapita ni jirani na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ambayo pia inatakiwa kulindwa ili isiharibiwe na shughuli za kibinadamu.

Aidha ameipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kuamua kuijenga Barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani ni muhimu kwa ajili ya wananchi kusafirisha mazao mbalimbali ambayo wanazalisha kwenye eneo hilo

Amesema mbali na umuhimu huo kwenye usafirishaji wa mazao pia ni muhimu kwa ajili ya kuwaunganisha wananchi wa Wilaya za Rungwe na Kyela Wilaya ya Makete mkoani Njombe.

Hata hivyo Dkt. Gwamaka amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo ikiwemo shughuli za kilimo.

Mwisho.