Site icon A24TV News

SERIKALI YAOMBWA KUSHUGHULIKA NA NG’OS ZINAZO TESA WAFUGAJI NGORO NGORO KWA MASLAI YAO BINAFSI

Na Geofrey Stephen

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Mimutie Women Organization limeiomba serikali kuchukua hatua kali kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayochochea migogoro ya ardhi wilayani Ngorongoro mkoani Arusha .

Aidha shirika hilo limeiomba serikali kukaa meza moja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, NGO’s na Wananchi waishio wilayani humo kujadili mgogoro usiokoma wa mipaka ambao unaendelea kuwaumiza jamii ya kifugaji hasa wanawake na watoto

Mkurugenzi wa shirika hilo, Rose Njiro alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Arusha na kusema kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua kali kwa NGO’s Pamoja na wanasiasa wakiwemo madiwani ambao wamekua ni changamoto kuzikichochea migogoro ya ardhi wilayani humo.

Njiro alisema migogoro ya ardhi imekuwa kikwazo cha maendeleo ya Wananchi wa jamii ya kifugaji na imekuwa neema kwa mashirika yasiyo ya kiserikali pwmoja na wanasiada  wanaoutumia mgogoro huo kujinufaisha kwa kufadhiliwa na mashirika ya nje kupata fedha na kuwasaliti wananchi pamoja na kuwadanganya

Alisema ipo haja kwa serikali kukutana na waathirika wa migogoro hiyo ili kuwajengea uwezo na kuleta mahusiano mazuri kati yao na mamlaka za uhifadhi ili kujua mipaka na kuiheshimu.

Mkurugenzi huyo alisema baadhi ya mashirika yamekuwa na ushawishi mkubwa kwa jamii za kifugaji na hivyo kuwajengea imani potofu Wananchi ili waichukie serikali, wawekezaji pamoja na mamlaka za hifadhi.

Alisema shirika hilo limefanya utafiti na kuibaini migogoro hiyo imekuwa na athari kubwa kwa wanawake na watoto na hivyo kuiomba serikali kukaa meza moja na makundi hayo ili kufikia mwafaka.

Kwa kutambua hayo shirika hilo limeamua kutumia mkutano wa 77 wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu unaoendelea jijini Arusha kupaza sauti zao na kulaani watu wachache walioigeuza migogoro ya Ngorongoro kama fursa ya kujiingizia kipato kutokana na fedha za wafadhili.

“Suala la Mgogoro Wilaya ya Ngorongoro limekuwa na athari kubwa kwa makundi maalumu ,wanawake,watoto na vijana na baadhi wa watu wanatumia migogoro hiyo kama fursa ya kujipatia kipato.” Amesema

Njilo ameiomba serikali kuangalia namna ya kukutana na jamii hiyo inayoteswa na migogoro isiyoisha ili kurudisha tumaini hususani kwa wanawake na watoto ambao wamekuwa wakiishi kwa mateso makubwa kutoka na mifugo yao kukamatwa na kutozwa faini kubwa.

Alifafanua kwamba septemba 19 mwaka huu Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha ilitoa uamuzi katika shauri namba 21 la mwaka 2022 ambapo wananchi watano walifungua shauri Mahakamani dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na mwanasheria wa serikali wakipinga uamuzi wa kumegwa kwa eneo wanaloamini ni mali yao ili kuwa pori tengefu la pololeti.

Alisema maamuzi ya Mahakama chini ya jaji Tiganga yaliamua kuwa eneo hilo litabaki kuwa eneo tengefu  kwa kuzingatia masharti yote ya mapori tengefu yataendelea kufuatwa ikiwemo kutoingiza mifugo.

Alisema maamuzi hayo yalitafsiliwa vibaya kwa wanasiasa na  Wananchi ambao walianza kuingiza mifugo yao kwenye eneo hilo na kujikuta mifugo yao ikikamatwa na kutozwa faini kubwa na hivyo baadhi yao kufilisika

Mwisho .