Site icon A24TV News

Takwimu sahihi ni muhimu katika ujenzi wa uchumi shindani wa Viwanda

Na Mwandishi wa A24Tv .

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashata Dkt Hashil Abdallah amewasihi wamiliki wote wa sehemu za shughuli za Kiuchumi na Kijamii ikiwemo wamiliki wa viwanda wote nchini kutoa ushirikiano unaohitajika katika kufanikisha Utafiti wa shughuli za kiuchumi na kijamii wa mwaka 2023 Tanzania Bara na wasiwe na hofu ya utoaji wa taarifa kwa kuwa taarifa hizo ni kwa matumizi ya kitakwimu kwa manufaa mapana ya watanzania kwa ujumla.

Ameyasema hayo Oktoba 29, 2023 akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji(Mb.) wakati wa kufungua mafunzo ya wasimamizi na wadadisi wa utafiti wa shughuli za kiuchumi na kijamii wa mwaka 2023 Tanzania Bara yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Ualimu (DUCE) jijini Dar es Salaam

Aidha, Amewaasa washiriki hao 527 wakiwemo Wasimamizi 27 na Wadadisi 500 kutoka Tanzania Bara
kuwa wavumilivu, wenye heshima na adabu ili wawwze kupata ushirikiano katika kukusanya takwimu sahihi na zenye ubora kwa kuzingatia mafunzo waliyopewa na kuwa na timu nzuri inayoshirikiana.

Vilevile Dkt. Abdallah amewataka Washiriki hao kuhakikisha wanakusanya taarifa zinakidhi malengo yaliyokusudiwa na zitakuwa kamilifu ili kuiwezesha Serikali kutunga sera, kupanga mipango, na kufuatilia utekelezaji wa program mbalimbali za maendeleo

Aidha amebainisha kuwa utafiti wa takwimu hizo unatarajiwa kusaidia katika utekelezaji wa malengo ya Mpango wa Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals- SDGs) na kupima hali ya mtawanyiko wa shughuli za kiuchumi nchini pamoja na Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) 2021/22 – 2025/26.

“Tunafahamu bidhaa nyingi tunazotumia zikiwemo za chakula zinachakatwa viwandani; hivyo, uzalishaji unatakiwa kuwa wenye staha na endelevu. Kama nchi hatuwezi kufikia lengo hili ifikapo mwaka 2030 ikiwa hatuna takwimu sahihi mnazoenda kukusanya na zitakazokusanywa baadae kutoka na Mhimili wa Sampuli itakayotokana na Utafiti huu”. Amebainisha Dkt Abdallah.

Dkt. Abdallah pia ametoa rai kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuwa Utoaji wa Takwimu Bora uwe changamoto muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Utafiti huu kwa kutumia Mpango Mkakati wa Kuboresha Utoaji Takwimu sahihi nchini ili kujenga uchumi wa viwanda hususani kuongeza thamani mazao na huduma uliojikita katika maeneo matatu ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani; kilimo, uchimbaji madini na viwanda vingine vya uchimbaji; na huduma.

Mwisho .