Site icon A24TV News

TCRA YAENDELEA KUPAMBANA NA MATAPELI WA TUMA KWA NAMBA HII LAINI ZAFUNGIWA MKURUGENZI MKUU AWATAKA WANCHI KUTOA USHIRIKIANO

Na Geofrey Stephen Arusha
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA ,imezifungia laini za simu zipatazo 34,848  zinazodaiwa kuhusika na uhalifu katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA  Dkt Jabir Bakari amebainisha hayo jijini Arusha wakati akiongea na vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa sekta ya mawasiliano katika kipindi cha Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24.
Alisema kuwa  laini za simu zilizofungwa ni zile zilizoripotiwa kupotea ,kuibiwa au kuhusika katika matukio ya uhalifu ikiwemo wizi na utapeli
Hata hivyo alisema idadi ya laini zilizofungwa katika kipindi hicho imeshuka kwa asilimia 11.5 kutoka laini 39,394 kwa takwimu za mwezi juni 2023.
Aidha alisema katika kipindi hicho cha Julai hadi Septemba simu zipatazo 23,328 zilibainika kuhusika na matukio ya ulaghai au uhalifu ikilinganisha na simu 23,234 za mwezi Aprili hadi juni mwala huu.
‘Ukilinganisha matukio ya mwezi julai hadi septemba utaona kuwa matukio ya uhalifu wa simu umepungua kidogo ukilinganisha na mwezi April hadi Juni hii ni kutokana na elimu juu ya matumizi ya namba 15040 ya kuripoti namba za wahalifu”
Akiongelea mawasiliano ya simu hapa nchini katika kipindi cha mwezi Septemba ,dkt Bakari alisema idadi ya watumiaji imeongezeka kwa asilimia 4.86 na kufikia laini milioni 67.12 kutoka laini 64.01 za mwezi Juni mwaka huu.
“Idadi hii ya laini za simu inahusisha laini kutoka mitandao 6 ya watoa huduma ambayo ni Airtel,Vodacom,Halsted,Ttcl,Tigobna Smile”.
“Takwimu za sasa pia zinaonesha kuongezeka kwa watumiaji wa Intaneti kwa asilimia 1.24 kutoka watumiaji 34,047,407 mwezi juni mwaka huu hadi kufikia watu 34,469,022 mwezi septemba mwaka huu”
Alisema ongezeko hilo limetokana na uwepo wa maudhui ya kiswahili kwenye  mtandao ikijumuisha kuongezeka kwa programu-tumizi kwa lugha ya Kiswahili.
Akizungumzia matumizi ya miamala ya fedha kupitia mitandao ya simu za mkononi katika kipindi cha robo ya mwaka ,dkt Bakari alisema takwimu zinaonesha kuwa akaunti za simu zimeongezeka  kutoka 47,275,660 mwezi juni na kufikia akaunti 51,369,347 mwezi septemba mwaka huu ,sawa na ongezeko la asilimia 8.7.
Alisema katika katika kipindi hicho miamala ya fedha imeongezeka kutoka 420,675,884 kwa kipindi kilichoishia  mwezi juni hadi miamala 422,390,546 kufikia septemba mwaka huu 2023.
Wakati huo huo dkt Bakari alisema kuwa jumla ya watoa huduma wa vituo vya radio vipatavyo 80 vimechukuliwa hatua ikiwemo kutozwa faini, onyo na adhabu kutokana na kukiuka wa taratibu za utoaji wa maudhui..
Aidha aliongeza kuwa TCRA kwa kushirikiana na wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake na makundi maalumu, imekamilisha uratibu wa programu maalumu ya kuandaa vipindi vya maadili vitakavyorushwa na vituo vya Utangazaji  vipatavyo 150 vyenye leseni ya kiwilaya.
Alisema mpango huo umelenga kutoa elimu na kujenga jamii inayozingatia maadili ,mila ,destuli na Utamaduni wa mtanzania.
Mwisho