Site icon A24TV News

WAZIRI MKENDA VYUO VIKUU HAVIPIMWI KWA WINGI WA WANAFUNZI BALI NI TAFITI ZENYE UGUNDUZI KWA JAMII

Na Mwandoshi wa A24Tv

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Vyuo vikuu havipimwi kwa wingi wa wanafunzi na mapato badala yake tafiti inazofanya zenye kuleta gunduzi, kukuza maarifa na ujuzi katika jamii.

Prof. Mkenda amesema hayo jijini Dodoma wakati akizindua Baraza jipya la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kutoa wito kwa Vyuo vikuu kuzingatia ufanyaji wa tafiti zenye tija nchini ili kuchochea ushindani katika gunduzi mbalimbali ndani na nje ya nchi

“Vyuo vikuu havipimwi kwa wingi wa wanafunzi na wingi wa mapato, kuna vipengele vingi vya upimaji ubora wa elimu ya chuo kikuu mojawapo ni ufanyaji wa tafiti. Lazima Chuo Kikuu kiwe chemchem ya kuvumbua na kutafuta majibu ya changamoto za wananchi kwa kufanya tafiti,” amesema Prof. Mkenda

Ameongeza kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo vyetu ni vyema zikashindanishwa kimataifa ili ziweze kuwa na viwango vya ubora zaidi katika nyanja za kimataifa ili kuvifanya vyuo vyetu viwe na uwezo wa kufanya kazi na watu wa mataifa mbalimbali duniani.

” Hivi karibuni Wizara imetoa tuzo na fedha kwa watafiti ambao wamechapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida ya kimataifa kama motisha lakini pia kuwafanya watafiti wa Tanzania kushindana kimataifa, Niwapongeze OUT kwa kazi nzuri ya kuendelea kuzalisha wataalamu na kufanya tafiti, mhadhiri mmoja kutoka chuo hiki amepata tuzo hongereni,”amesema Prof. Mkenda.

Amesema Chuo Kikuu ni mahali pa kuzalisha wataalamu na wabobezi ambao wakitoka wanakwenda kufanya kazi za kutoa huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Joseph Kuzilwa, amemhakikishia Waziri Mkenda kuwa baraza jipya lililoteuliwa ni la watu wenye taaluma na ujuzi wa kutosha kuweza kusogeza ambele gurudumu la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema baraza hili jipya limepata fursa ya mafunzo ya siku tatu ambapo wawezeshaji watatoa mada mbalimbali zitakazowajengea wajumbe uwezo zaidi ili waweze kutimiza wajibu wao vizuri na kwa ufanisi.

Mwisho .