Site icon A24TV News

DC ARUSHA, AKAMATA LITA 1780 ZA UWIZI WA MAFUTA YA MAGARI YA SERIKALI PETROL NA DIZEL ENEO LA NJIRO ARUSHA

Na Geofrey Stephen Arusha.

Katika operesheni ya kimya kimya Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Mtehengerwa kwa kushirikiana na jeshi la Polisi jijini hapa,wamekamata lita 1785 za Mafuta ya Petroli na Dizeli,yanayodaiwa kuibwa na madereva wa serikali pindi wanapoenda kuweka mafuta kwenye  magari ya serikali.

Akiongea mara baada ya operesheni hiyo Mtehengerwa alisema kuwa mafuta hayo yalipatikana baada ya taarifa za siri za msamalia wema ,yakiwa yamefichwa kwenye nyumba moja iliyopo mtaa wa Kambarage katika kata ya Themi jijini Arusha huku mtuhumiwa Jofrey Makala akifanikiwa kutoroka.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akinunua mafuta hayo kutoka kwa madereva wa serikali wasio waaminifu kwa lengo la kuihujumu serikali pindi  wanapoenda kujaza kwenye vituo vya mafuta .
“Mbinu inayotumiwa na madereva wa magari ni kutembea na vidumu kwenye gari na wakati wanaweka mafuta yaliyokusudiwa huweka nusu kwenye gari na mengine huweka kwenye dumu na risiti inayotoka kwenye mashine huonesha idadi ileile  iliyokusudiwa na baadaye wanakuja kuuza kwa mtuhumiwa”
Alisema taarifa za uwepo wa biashara hiyo alizipata kutoka kwa wasamalia wema ambapo aliamua kufuatilia kwa kuweka mitego na kufanikiwa kukakata mafuta hayo huku mtuhumiwa akifanikiwa kutoroka.
“Tumepata taarifa kwa wasamalia wema kuna bwana anaitwa Jofrey Makala ambaye kazi yake ni kununua mafuta ya petro na Dizeli kutoka kwa madereva wa serikali na madereva wa makampuni mbalimbali na kuyaficha katika nyumba hiyo na baadaye kuyauza kwa wafanyabiashara kwa kweli tumekuwa tukihujumiwa kama serikali .
“Baada ya kupata taarifa hiyo ilitulazimu tulifuatilia kwa siku kadhaa na baadaye tulikuja kufanya ukaguzi wa kushtukiza tukijifanya sisi ni wateja na tulipofika Jofrey makala alitushtukia na kuondoka lakini msaidizi wake alitufungulia na kudhani sisi ni wateja”.
Alisema baada ya kufika ndani ya eneo hilo walikuta idadi kubwa ya madumu ya lita 20 na waliamua kuchungulia ndani ya nyumba hiyo na kuona idadi kubwa ya madumu.
“Tulilazimika kuita vyombo vya dola ,viongozi wa mtaa pamoja na mashuhuda na walipofika tulilazimika kuvunja mlango na kuingia ndani, tulikuta idadi kubwa ya madumu ya lita 20,lita 5 na lita 10 yakiwa na mafuta na mengine yakiwa matupu “
Alisema baada ya madumu hayo kutolewa nje na kuhesabiwa ilibainika yalikuwa na lita 1785 ya dizel na petroli huku madumu tupu ni zaidi ya 120 ambayo yalipakiwa na kupelekwa kituo cha Polisi
Mkuu huyo alitoa rai kwa Taasisi za serikali na makampuni ya umma kufuatilia matumizi ya mafuta wanayopewa  madereva na kuwataka madereva wa serikali wanaojihusisha na uharamia wa kuihujumu serikali waache mara moja.
Pia aliwataka wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya kuiibia serikali waache mara moja kwani hawatakuwa salama na huyo mtuhumiwa  ajisalimishe mara moja kituo cha Polisi.
Naye mjumbe wa serikali ya mtaa wa Kambarage Maria Chakachaka,alisema tukio hilo limewashtua na sasa wanajipanga kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye majumba yanayohifadhi bidhaa(Godauni) ili kubaini kilichomo.
Alisema awali hawakuwa na taarifa ya biashara inayoendelea katika nyumba hiyo kwani walikuwa wakiona watu wanaingia na kutoka bila kujua wanafanya biashara gani ila kqa sasa watafabya ukaguzi wa kina maeneo yasiyoeleweka.
Mwisho .