Site icon A24TV News

MUGODI WA BUCKREEF UNAZALISHA DHAHABU YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 8 KWA MWEZI DKT. KIRUSWA

Na Richard Mrusha

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameutaka Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef kuhakikisha unatenga kiasi cha dhahabu kwa ajili ya kusafisha kwenye viwanda vya ndani au kuuza katika masoko ya ndani ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo imeanza kununua dhahabu kwa ajili ya akiba.

Ametoa rai hiyo leo Novemba 13, 2023 mkoani Geita alipotembelea mgodi huo kukagua maendeleo ya shughuli za uzalishaji pamoja na kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazoukabili mradi huo.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa Serikali imeamua kutumia dhahabu inayozalishwa hapa nchini ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kwa kuhakikisha Benki Kuu ya Tanzania inakuwa na akiba ya dhahabu lakini pia dhahabu inayozalishwa hapa nchini inasafishwa katika Viwanda vya kusafisha madini hayo hapa nchini.

“Mmesema hapa kuwa mmeingia mkataba wa manunuzi ya dhahabu na kampuni ya kigeni, hakikisheni mnatenga kiasi cha dhahabu kwa ajili ya kuuza au kusafisha katika viwanda vya ndani, ni kwasabbu ili tuwe na akiba ya kutosha ya fedha kigeni, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza nchi iwe na akiba ya dhahabu inayozalishwa hapa nchini na tayari Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iko kwenye mchakato wa kuweka akiba ya dhahabu kiasi kisichopungua tani 6 kwa mwaka, na hiyo dhahabu itatoka kwa wachimbaji wakubwa, Kati na wadogo na nyie mnaweza kuuza kwao” amesema Dkt. Kiruswa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameutaka mgodi huo kusaidia wananchi wanaozunguka mradi huo kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii kujenga miradi endelevu ili hata pale shughuli za uchimbaji zitakapofikia ukomo wakazi hao waendelee kunufaika na miradi hio endelevu.

“Nimesikia hapa kuwa mmetoa zaidi ya shilingi milioni 400 kwenye miradi kama CSR, niwahimize mtengeneze miradi endelevu ili hawa wananchi waliopisha mradi wenu wapate kuona manufaa ya uwepo wa rasilimali hii, nafahamu mmesaidia upande wa huduma za kijamii kama elimu na afya, nawapongeza kwa hilo lakini pia hili la miradi endelevu mlichukue mkalifayie kazi mtengeneze hizo fursa ili manufaa ya mgodi yabaki kwa mud mrefu” amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Gaston Mjwahuzi amesema kuwa Mgodi umepokea maelekezo ya Naibu Waziri Dkt. Kiruswa na kwamba watatekeleza kwa kuwa ni manufaa ya taifa na uchumi kwa ujumla.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Mjwahuzi amesema kuwa hivi sasa mgodi unazalisha wakia tani 1700 hadi 2000 kwa mwezi ambako wanazalisha dhahabu yenye thamani ya shilingi bilioni 8 kwa mwezi

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Geita Kara Magaro ameushukuru mgodi huo kwa kujenga miradi ya huduma za kijamii yakiwemo madarasa na zahanati ambako tangu mradi huo uanze tayari kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 400 zimetolewa na mgodi kama Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) na kusaidia kupunguza adha ya uhaba na uchakavu wa miundombinu katika sekta ya elimu na afya katika Halmashauri hiyo.

Mwisho .