Site icon A24TV News

Ongezeni kilimo cha miwa kwa Wingi-Dkt.Kijaji.

Na Mwandishi wa A24tv.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt.Ashatu Kijaji(Mb) amewasihi wananchi na wakulima wa miwa wa Kata ya Magugu Wilaya ya Babati Mkoani Manyara kuongeza kilimo cha miwa kwa wingi ili kuweza kulisha kiwanda cha Sukari cha Manyara .

Dkt. Kijaji amebainisha hayo Desemba 28,2023 wakati alipotembelea Kiwanda hicho ili kujionea shughuli za uzalishaji na changamoto za Kiwanda hicho kwa lengo la kuzitatua na kuongeza uzalishaji wa bidha muhimu ya sukari Nchini.

Dkt. Kijaji amesema kuwa ni wakati sasa wa wananchi na wakulima wa miwa kuongeza kasi ya kilimo cha miwa ili kuweza kukipa nguvu Kiwanda cha Sukari cha Manyara ili kuondokana na upungufu wa malighafi ya miwa inayoendelea katika kiwanda hicho pamoja na kukabiliana na upungufu wa sukari,bei kupanda pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi.

Aidha amesema katika kukabiliana na changamoto ya maji Serikali imeandaa Mpango wa visima Zaidi ya 680 ambapo 150 vitachimbwa katika Wilaya ya Babati na ameelekeza Kata ya Magugu ipatiwe kipaumbele katika uchimbaji wa visima hivyo hususani kwenye mashamba ya miwa.

Hata hivyo ameuagiza uongozi wa Kiwanda hicho kuandaa mpango wa muda mrefu ikiwemo uchimbaji wa mabwawa makubwa yatakayosaidia kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji ili kuwaondolea wakulima wa miwa utegemezi wa msimu wa mvua pekee.

Vilevile Dkt. Waziri ametoa rai kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa wazalendo na wenye kujituma pamoja na kufanya kazi kwa ufanisi ili kuongeza uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe.Lazaro Twange amesema kuwa Mkoa utaendelea kushirikiana na Uongozi wa Kiwanda hicho ili kusaidia kuondoa changamoto mbalimbali na pia kutekeleza maagizo yote ya Serikali yaliyotolewa ili kusaidia kilimo cha miwa katika kata ya Magugu.