Site icon A24TV News

Taasisi zinazohusika na Mradi wa Magadi Soda – Engaruka zatakiwa kushirikiana kuwezesha mradi huo kuanza

Na Geofrey Stephen .Arusha

Serikali imewataka Viongozi wa Taasisi zinazohusika na Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka Wilayani Monduli Mkoani Arusha kushirikiana kwa karibu katika kukamilisha taratibu zote zinazohitajika ili Mradi huo unaotarajiwa kuongeza ajira, malighafi za viwandani, kukuza biashara na uchumi wa Taifa uanze kutekelezwa kwa wakati.

Hayo yamesemwa Desemba, 21,2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandubya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Bw. Kheri Mahimbali walipotembelea Mradi huo wa Kimkakati wa Magadi kwa lengo la kuona utekelezaji wake na kutatua changamoto mbalimbali zitakazowezesha kuanza kutekelezwa rasmi kwa mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika Mradi huo Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amesema Ziara hiyo imeshirikisha Wizara tatu, Taasisi nne na vijiji vinne katika kujadili mambo mbalimbali yanayohusu kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ambao utasaidia katika kuboresha maisha ya wakazi wa Engaruka na Taifa kwa ujumla, kuongeza mapato kwa Serikali.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Bw. Kheri Mahimbali amebainisha kuwa kuanza kuchimbwa kwa madini ya Magadi soda nchini kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitumika kuagiza Magadi soda kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya malighafi hiyo viwandani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo, (NDC) Dkt Nicolaus Shombe amebainisha kuwa NDC kama mwekezaji kwa niaba ya Serikali tayari imekamilisha hatua mabalimbali za kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kufanyika kwa upembuzi yakinifu pamoja na tathmini ya mazingira huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyouchukulia mradi huu kwa uzito wa kipekee na nia ya dhati iliyonayo ya kutaka kutekelezwa kwa mradi huu..

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mwl. Happyness Laizer pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli Muhsin Kassim wamesema wapo tayari kupokea mradi huo huku wakitoa rai kwa wananchi kuchangamikia fursa zitakazotokana na utekelezwaji wa Mradi huo.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa Engaruka Viongozi wa eneo hilo wakiwemo Diwani na Mtendaji wa Kata ya Engaruka pamoja na Wenyeviti wa Vijiji vya Engaruka juu, Engaruka chini, Irerendeni pamoja na Oldonyo Lengai wameonyeshwa kufurahishwa na hatua ya Serikali kuamua kutekeleza mradi huo utawakaowaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani katika upatikanaji wa ajira, ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.

Mradi wa Magadi soda wa Engaruka ni moja kati ya miradi kumi na saba ya kimkakati ya Serikali ambao upo chini ya Shirika la Taifa la Maendeo (NDC) ambao unaelezwa kuwa utekelezwaji wake utakuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa Taifa kwa kuwa utasaidia katika kutoa malighafi mbalimbali za Magadi soda kwa viwanda ndani na nje ya nchi, kutoa ajira elfu moja za moja kwa moja kwa wananachi ambapo uwekezaji wake unatarajia kugharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni mia nne.

Mwisho .