Site icon A24TV News

VIJANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA AJIRA KATIKA KIWANDA KIPYA CHA KUUNGANISHA MAGARI

Na Mwandishi wa A24Tv .

Waziri wa Vjwanda na Biashara Mhe. Dkt Ashatu Kijaji(Mb) ametoa rai kwa vijana wa Tanzania kuendelea kujielimisha na kupata ujuzi mbalimbali ili kuwa tayari kuajiriwa na viwanda mbalimbali vinavyoendelea kujengwa nchini kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza nchini hususani katika kujenga viwanda.

Ameyasema hayo Desemba 11, 2023 alipotembelea Kiwanda cha Saturn Corporation limited kilichopo Kigamboni Dar es salaam lengo la kuangalia ujenzi unaoendelea katika Kiwanda hicho kinachounganisha magari ya SINOTRUCK aina ya Howo na Tipper

“Tuliahidi uko nyuma na Mheshimiwa Rais amesema hata juzi wakati wa uzinduzi wakuandika Dira yetu ya Taifa 2050 kwamba 2025 tulitamani kuona Tanzania ya viwanda, tulitamani kuona Tanzania inafikia uchumi wa kati kiwango cha juu Kiwanda hiki ni moja ya ushahidi kwamba yale anayo yasema Mheshimiwa Rais yanauhakika na tunaendelea kusimamia kuona taifa letu la uchumi wa viwanda linaonekana na uchumi wetu wakati tunaweza kuufikia mwaka 2025” Dkt Ashatu Kijaji

Dkt.Kijaji amesema kiwanda hicho cha kuunganisha magari kitatumia malighafi za vioo kutoka viwanda vya ndani na kinatarajiwa kuuza bidhaa zake ndani ya soko la EAC na Afrika na hivyo kuchangia kukuza biashara na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Naye Mbunge wa Kigamboni Dkt Faustine Ndugulile amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza wilayani humo kwa kuwa iko tayali kuwasaidia kupata maeneo na vibali mbalimbali vinavyohitajika pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara, umeme na maji.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kiwanda hicho Bw. Rehmatullah Habib Mouna amesema kiwanda hicho kikubwa Afrika Mashariki na Kati kitaanza kufanya kazi rasmi Machi 15, 2024 na ameomba watanzania wasomi kujitokeza hasa wahandisi kwenda kujifunza taaluma mpya ambayo italeta muamko kwa watanzania.

” Tumetoa ajira kwa Watanzania hadi sasa watu 150 katika kampuni yetu lakini kwa hali inavyoenda tutaongeza ajira ili shifti zifanyike kwa ziada” Rehmatullah.

Mwisho .