Na Geofrey Stephen Monduli.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kilimatinde Wilayani Arumeru Mkoani Arusha na wananchi wa Kijiji cha Moita Bwawani Wilayani Monduli wanamtuhumiwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Moita Bruno Mollel kwa kumega ardhi ya malisho ekari 3,000 kuwa eneo la makazi bila ridhaa ya wananchi.
Wakizungumza katika Mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na watu zaidi ya 150 uliofanyika katika Kijiji cha Moita Bwawani walisema na kuiomba serikali kusitisha zoezi hilo kwa kuwa Mwenyekiti Mollel hajali wananchi wenye mifugo kwani eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Mollel alisema ardhi ni ya watanzania wote na sio ya baadhi ya vijiji hivyo wao wanaungana na wananchi wa vijiji vingine kupinga kumegwa kwa ardhi hiyo ili eneo hilo liendelee kuwa eneo la malisho na sio vinginevyo.
Naye Mwanakijiji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Ndekui Laizer yeye alisema kuwa utaratibu uliotumia Mwenyekiti Mollel wa kumega ardhi kwa ajili ya makazi sio sahihi kwani hakujali na kuzingatia maslahi ya wafugaji juu ya kutengwa eneo hilo kwa ajili ya malisho.
Alisema Mwenyekiti ameweka mbele tamaa zake na masilahi yake binafsi bila kuzingatia jamii anayoiongoza inayojali eneo la malisho kuliko makazi hivyo maazimio yote yaliyopitishwa yanapaswa kusitishwa na kubadilishwa kwa maslahi ya wananchi wa vijiji vyote vya Arumeru na Monduli.
Akijibu tuhuma hizo,Mwenyekiti Mollel alisema chokochoko zote za wananchi wa Kilimatinde na Moita zinachochewa na mwanasiasa na mfanyabiashara wa madini,Sanare Mollel na kudai kuwa maamuzi ya wengi yamezingatia na ndio maana serikali ilitoa hati ya ardhi kwa ajili ya kumega eneo la malisho kwa ajili ya makazi.
Mollel alisema kuwa vikao vya kijiji na halmashauri ya Kijiji vilikaa na kupata Baraka ngazi ya wilaya hivyo wale baadhi ya wote wanaopinga utoaji wa ardhi kwa ajili ya makazi hawana hoja za msingi kwa kuwa serikali ilishabariki na hatimaye kuridhia utoaji wa ardhi hiyo.
Akijibu tuhuma za Mwenyekiti kuwa yeye anachochoe vurugu za kupinga utoaji ardhi ya malisho kwa ajili ya makazi Mfanyabiashara Sanare Mollel alisema ni hoja dhaifu zisizo na mashiko na kusema kuwa wananchi wenye wameamua kutetea eneo hilo kwa ajili ya malisho.
Mollel alisema watanzania wa sasa hususani wafugaji wa jamii ya kimasai wamekuwa welevu na wenye kujitambua na kujua thamani ya eneo la malisho hivyo kumega kwa ajili ya makazi sio hoja yenye mashiko kwani taratibu zote hazikufuatwa hivyo aliiomba serikali kuhakikisha hilo linasitishwa kw amaslahi ya wananchi wa Moita na vijiji vya jirani.
Mfanyabiashara huyo aliwataka viongozi wa Kjiji cha Moita kujibu hoja za wananchi na sio kumsingizia yeye eti naleta chokochoko na vurugu kwani wananchi wa jamii ya kifugaji wanajali eneo la malisho kuliko makazi.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli aliyetambuliwa kwa Anaeli Mbise aliwaeleza wananchi hao kuwa suala lao liko mikononi mwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli,Joshua Nassari na kusema kuwa atakuja siku ya ijumaa desemba 14 mwaka huu kutoa maelekezo ya serikali.
Mwisho