Na Mwandishi wa A24tv .
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) alitoa wito kwa Watanzania kuacha kununua bidhaa zinazotoka nje ya nchi Ilihali zinazalishwa nchini na kwa viwango vyenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
Aliyasema hayo Januari 6,2024 Dar es Salaam baada ya kutembelea Viwanda vya Motisun (IMMI Steel) vinavyozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo bati, nondo, plastiki, juisi na rangi.
Aidha Dkt. Kijaji pia alosema vipo viwanda nchini vinavyozalisha bidhaa zenye ubora unaostahiki na kwamba Watanzania waache kukimbilia nje ya nchi,badala yake wanunue bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Tanzania ina viwanda vinavyotengeneza bidhaa nzuri zisizo na mashaka, bidhaa hizo zina viwango vyote vinavyotakiwa na Taasisi za ukaguzi,” alisema Dk Kijaji.
Aidha, aliongeza kuwa wakati Taifa likielekea kwenye Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 ni vyema kuona namna ya kulinda viwanda kwa manufaa ya Watanzania.
Vilevile aliwashauri wenye viwanda kuwa wavumilvu kwenye changamoto ya umeme na kwamba ni kwa kipindi kifupi na ifikapo Februari 2024 kama ilivyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan suala hilo litafikia mwisho.
Alisema Tanzania inaonuwezo wa kuzalisha bidhaa inayokidhi viwango vya juu kabisa ambapo ni wakati sasa wa kuieleza Dunia juu ya bidhaa hizo ambazo zinakidhi mahitaji ya soko
Wakati huo huo ,Dkt. Kijaji alitumia muda huo kuwahamasisha wenye viwanda hao kujipanga kupeleka bidhaa zao katika masoko mengi nje ya nchi ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)na Eneo huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Mwisho .