Site icon A24TV News

MAHAKAMA KUU YAPIGA HATUA KATIKA USIKILIZWAJI WA KESI NCHINI.

Na Geofrey Stephen Arusha.

Mahakama imepiga hatua kubwa katika usikilizaji wa mashauri hususani mashauri ya mlundikano kutoka asilimia tano (5) kwa mwaka 2022 hadi kufikia asilimia mbili (2) kwa mwaka 2023.

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ameyasema hayo jijini Arusha wakati akitoa maneno ya utangulizi akimkaribisha Mgeni Rasmi Jaji Mkuu wa Tanzania katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Tangu mwaka 2022 ambapo kikao kama hiki kilifanyika hali ya utoaji haki kwa Mahakama Kuu imekuwa bora zaidi.

Aidha amesema kuwa, muda wa wastani unaotumika tangu shauri kufunguliwa mpaka kumalizika umepungua kutoka siku 321 mpaka 262. Pili, idadi ya mashauri ya mlundikano imepungua kutoka asilimia 5 mpaka asilimia 2, yaani kutoka kesi 896 mpaka 262.

Kadhalika Jaji Kiongozi amebainisha kuwa, katika Mahakama za chini nayo imezidi kuwa bora ambapo muda wa wastani ambao mashauri yanatumia katika Mahakama za Hakimu Mkazi umepungua kutoka siku 302 hadi 235 na katika Mahakama za Wilaya umepungua kutoka siku 159 mpaka siku 120.

Vivyo hivyo, Jaji Kiongozi ameeleza kuwa, idadi ya kesi za mlundikano katika Mahakama hizo imepungua kutoka mashauri 878 mpaka 455 katika Mahakama za Hakimu Mkazi, kutoka mashauri 915 mpaka 706 katika Mahakama za Wilaya na kutoka mashauri 19 mpaka 0 katika Mahakama za Mwanzo.

Aidha, amesema, pamoja na kwamba kasi ya wastani wa umalizaji wa mashauri imeongezeka na kupungua kwa idadi ya mashauri ya mlundikano amesema ni vema kujiuliza kama bado ni sahihi muda wa shauri la mlundikano kubakia miezi 24 kwa Mahakama kuu, miezi 12 katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya na Miezi sita katika Mahakama za Mwanzo au kama ni wakati sasa wa kutafakari upya muda wa shauri kuwa la mlundikano.

Aidha Mhe. Siyani amesema kuwepo kwa viwango vya idadi ya mashauri ambayo Majaji na Mahakimu wanapaswa kuyaamua kwa mwaka, kumeonekana kuiweka hai dhana ya utoaji haki kwa wakati.

“Dhana ya kupanga idadi ya mashauri ya kusikiliza kwa Majaji na Mahakimu inaendelea kuonyesha umuhimu wa kutiliwa mkazo na kusimamiwa kwa viwango hivyo. Katika kikao hiki, pamoja na mambo mengine, tutaendelea kukumbushana juu ya kutimiza, na kusimamia utimizwaji wa viwango hivyo ili kuiishi dhima ya utoaji haki kwa wakati na kwa wote,” ameeleza.

Lengo la kikao cha Majaji Wafawidhi ni kujipima na kujitathmini juu ya utendaji kazi sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto na kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

Mada zitakazotolewa katika Mkutano huo wa siku tatu (3) ni pamoja na utekelezaji wa maboresho ya huduma za Mahakama, malezi ya kitaaluma, namna bora ya kukabiliana na mabadiliko (change management), majukumu ya Majaji Wafawidhi katika usimamizi wa shughuli za Mahakama na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo (stress management

Mwisho.