Site icon A24TV News

SERIKALI KUBORESHA HOSPITAL YA ALMC ,MAKAMU WA RAIS AMPONGEZA ASKOFU MPYA ,BARA BARA YA LAMI YANUKIA KANISALA LA KIMANDOLU

Na Geofrey Stephen Arusha .

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema, serikali inajivunia ushirikiano mzuri uliopo kati yake na taasisi za dini ambao umedumu kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali na inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa katika utoaji wa huduma za jamii, hususan elimu, afya na maji.
Aidha ameiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha inatatua changamoto zinazokwamisha ubia baina ya serikali na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center kutatuliwa haraka iwezekavyo.
 
Dkt Mpango amebainisha hayo wakati aliposhiriki Ibada ya kuwekwa Wakfu na Kuingizwa kazini kwa Askofu Mteule Dkt Abel Godson Mollel na msaidizi wake Mchungaji Lareiton Lukumay iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Kimandolu mkoani Arusha.
Alisema serikali itahakikisha wananchi wanaendelea kuabudu kwa Imani zao bila kuvunja sheria na kuishi kwa amani na kupata huduma bora za kijamii pamoja na kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta zote ambayo ikikamililika itachangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa Taifa.
Alisema pamoja na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya vijana bado muitikio wa vijana hao katika nyumba za ibada ni mdogo hali inayopelekea kukosa mafundisho ya dini ambayo yangewawezesha kuwa na maadili na matumizi bora ya mitandao ya kijamii.
Aidha Makamu wa Rais alisema Serikali inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wote itasimamia na kulinda katiba ya nchi ikiwemo haki ya kuabudu kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Makamu wa Rais amewasihi viongozi wote wa dini nchini kusaidia kutoa hamasa kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu. Amesema Serikali inaahidi kufanya jitihada za kuweka mazingira ya haki na wezeshi ili wananchi waweze kushiriki kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na utulivu.
Makamu wa Rais amewapongeza Askofu Dk Abel Godson Mollel na Msaidizi wake Mch. Lareiton Lukumay kwa kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini na kuwasihi waamini wa Dayosisi hiyo na Wakristo wote kwa ujumla kutambua wajibu waliyonao kwa Viongozi wa kiroho.
Aliwaasa waamini kumpa ushirikiano wa dhati ikiwa ni pamoja na kumpenda, kumtii, kumtia moyo na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu Askofu Dk Abel Mollel ili aweze kutenda vema kazi yake.
Kwa upande wake Askofu Dk Abel Mollel amesema Dayosisi hiyo itaendelea kushirikiana vema na serikali katika kutoa huduma za kijamii kama vile elimu na Afya. Ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano na Kanisa ambao umewezesha kufanikisha shughuli mbalimbali ikiwemio kupanda miti zaidi ya laki tatu katika mkoa huo.
Awali askofu mstaafu wa kanisa hilo dayosisi yà kaskazini kati aliyekabidhi kijiti,Solomon Masangwa aliwashukuru waumini wa kanisa hilo,serikali ya mkoa na taifa kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha uongozi wake wa takribani miaka 10 na kusema kuwa  mashirikiano
 hayo yaendelee kwa askofu mpya  aliyeingizwa kazini.
Aidha alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha demokrasia hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuilinda katiba .Alimpongeza rais kwa kuruhusu Maandamano ya upinzani ikiwa ni njia sahihi ya serikali yake kuwapa uhuru wananchi kufikisha ujumbe wao kwa njia ya amani
MWisho