Na Mwndishi wa A24tv .
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inaendelea kutoa kipaumbele kwa wanaosoma masomo ya Sayansi ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo ili kuongeza hamasa kwa Vijana wa kitanzania wakiwemo wasichana kupenda kusoma masomo hayo.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Februari 11, 2024 mkoani Arusha katika Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, ambapo amesisitiza kuwa serikali pia itaendelea kuwekeza katika mazingira mazuri kwa ajili ya Vijana kupata fursa mbalimbali katika nyanja za Sayansi za masomo na kuendeleza ubunifu ili kuendana na kasi ya teknolojia duniani na hata soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Taifa lina upungufu wa Wanasayansi na hasa Wanawake na Wasichana, kwa sababu ni wachache wanaosoma ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) hivyo tutaendelea kuhamasisha wasichana kupenda na kujiunga na masomo hayo”. Alisema Mkenda.
Ameongeza kuwa ili Taifa liendelee linahitaji Wanasayasi hivyo Wizara na Wadau mbalimbali wataendelea kufungua fursa na kuweka mazingira sahihi ya ujifunzaji katika Sayansi.
“Tutaendelea kuwahimiza na kuanza programu ya kuwatangaza Wanawake na Wasichana mahiri Wanasayansi ili kutoa hamasa na kuonesha wanaweza kusoma katika eneo la Sayansi leo tumemshuhudia mwanamama Mtanzania Prof. Najat mbobezi katika Sayansi ya Nyuklia hivyo inawezekana” alifafanua Waziri Mkenda.²
Alibanisha kuwa Serikali inatekeleza baadhi ya afua ili kuongeza idadi ya wataalam wa Sayansi Wanawake, ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili wa masomo ikiwemo Samia Scholarship_ na Mikopo, kujenga Shule za Sekondari Maalum za Sayansi za Wasichana kila Mkoa, kuimarisha mafunzo ya Ualimu wa Sayansi, kufanya mapitio ya sera ya sayansi Teknolojia na Ubunifu na kupitia mitaala mipya kutoa msukumo katika masuala ya kuwezesha wanafunzi kuwa na fikra tunduizi na kutoa kipaumbele katika somo la TEHAMA ambapo tutandaa wanasayansi wa kutuwezesha kwenda sambamba na mapinduxi ya nne ya viwanda
“Katika wanufaika wa Samia Scholarship asilimia 40 ni wasichana hivyo tutaongeza hamasa ili kuongeza idadi hii ifike 50 kwa 50 au hata zaidi. Kikubwa wasichana waongeze bidii kwa sababu vigezo vya Skolaship hii ni wale wanaofaulu kwa kupata alama za juu katika masomo ya Sayansi kidato cha Sita’’. Alibainisha Waziri Mkenda.
Mkurugenzi wa Elimu Endelezi kutoka Taasisi ya STEM katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) Dkt. Leonard Mwalongo ameishukuru Serikali Kwa kutoa ufadhili wa masomo ya Sayansi kwa Wasichana waliopungukiwa sifa za moja kwa moja za kujiunga na Vyuo Vikuu katika kozi za Sayansikupitia foundation program ya Mwaka mmoja inayotolewa na OUT.
“Ufadhili huu ni asilimia mia moja unatolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa miaka 5, tunatarajia kufadhili Wanafunzi 1,000 ambapo kila mwaka 200 watanufaika, “amesema Dkt. Mwolongo.
Awali akiwasilisha mada katika maadhimisho hayo Mzungumzaji Mkuu Prof. Verdiana Masanja amesema kuwa hapa Tanzania ni asilimia 12 pekee ya Wanawake wapo katika Uongozi wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM). Na kwamba ni wakati muafaka kuwahimiza Wasichana na Wanawake pamoja na kuweka mazingira kwa ajili ya kusaidia ukuaji wao katika masuala ya uongozi, taaluma na ujasiriamali bila kusahau kuwaandaa kuingia katika mapinduzi ya nne ya Viwanda yakisukumwa na teknolojia mpya ikiwemo _AI (Artificial Intelligence ) na IOT (Internent of Things)_
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi. Jovita Mlay ameshauri Vyuo vya Ualimu kufundisha kwa kutumia mbinu shirikishi kuweza kutoa Walimu bora wa Sayansi watakaoweza kufundisha masomo ya kwani bado kuna pengo kubwa hasa kwa wanawake.
Mwisho .