Na Doreen Aloyce , Dodoma
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo katika maandalizi ya kuunda timu ya wataalamu itakayoweza kutembelea taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku ikiwa ni kutekeleza agizo la Dkt.Rais Samia Suluhu Hassan la kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 2024.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Seleman Jaffo jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa ambapo amesema lengo la maelekezo ya Rais Samia ni Kupunguza madhara ya kiafya na Mazingira yanayosababisha na kukithiri kwa matumizi ya kuni na mkaa katika jamii.
“Mtakumbuka kuwa katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazoandaa na kulisha watu zaidi ya mia moja (100) kwa siku, ifikapo Januari, 2024,”amesema.
Amesema kuwa Taasisi hizo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Alieleza kuwa Taasisi hizo zilielekezwa kuwasilisha mipango yao ya kuhama kutoka matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Wizara zote zimetuma mipango husika ya matumizi ya nishati mbadala na jinsi zitakavyotekeleza agizo hilo na Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa kanzidata ya taarifa kutoka Wizara zinazotekeleza katazo hilo ili kuweza kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo,”amesema.
Aidha amesema kuwa Taasisi zote zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku, kupitia Wizara zenye dhamana na Taasisi hizo, zimetoa taarifa za utekelezaji wa agizo hilo ambapo katika Sekta ya Elimu,
utekelezaji wa agizo la Serikali umefanyika ambapo hadi kufikia tarehe 31 Januari 2024, jumla ya Vyuo vya Ualimu 30 kati ya 35 sawa na asilimia 85.71 ya lengo, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 51 kati ya 54 sawa na asilimia 94.44 ya lengo, na Vyuo vya Elimu ya Ufundi (VETA) vinane (8) kati ya 36 sawa na asilimia 22.22 vimeshaunganishwa na huduma ya Nishati mbadala ya Kuni Poa (Clean Energy Briquettes) na Gesi.
Hivyo serikali inaipongeza Wizara ya Elimu kwa kuwa kinara kwa taasisi zake nyingi kutekeleza agizo hilo la serikali kwa zaidi ya asilimia 85.
Ambapo amesema Taasisi zingine zinapaswa kuiga mfano mzuri uliofanywa na Wizara ya Elimu na Taasisi zake.
Hata hivyo amesema kuwa takwimu za uharibifu wa misitu nchini zinaonesha kuwa takriban hekta 469,420 za misitu zinapotea kila mwaka kutokana na matumizi yasio endelevu ya rasilimali za misitu ikiwemo uvunaji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
“Hali hiyo imekuwa ikisababisha madhara makubwa ikiwemo kupungua kwa vyanzo vya maji, kuwepo kwa vipindi virefu vya ukame na kupotea kwa bioanuai,”amesema.
Mwisho.