Akina Mama wa Kata ya Riroda wilayani Babati mkoani Manyara, wamesema wamechoshwa na vitendo vya kubakwa na kuporwa mali zao na watu ambao bado hawajafahamika hali inayowapa hofu ya kwenda maeneo ya mlimani kutafuta kuni.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na mkuu wa wilaya Lazaro Twange kwa lengo la kusikiliza kero na kuzitafutia majibu akiwa na idara mbalimbali, wamesema watoto wa shule pia wanakumbana na vitendo hivyo vya ukatili kwani wapo baadhi wamekatisha masomo yao kwa kupewa ujauzito na watuhumiwa hawajakamatwa mpaka sasa.
“Tukiamka salama tunashukuru Mungu, watoto wetu wa kike wakienda shule tunafofu, sisi twende wapi jamani, tunaogopa hata kwenda ,limani kukata kuni, alisema mmoja wa akina mama
Mmoja wa askari wa akiba Abdilah Hassan Said, amesema ukatili na wizi katika kijiji hicho unasababishwa na baadhi ya viongozi wa kijiji na vitongoji kijijini hapo kuwafumbia macho wauzaji wa pombe haramu aina ya Gongo na kusitishwa kwa askari wa akiba (mgambo) waliokuwa wakisaidia kufanya doria na kuwakamata wahalifu.
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amekemea vitendo hivyo na kuutaka uongozi wa kijiji kuvunja mitambo yote ya pombe haramu, kuwabaini wahalifu na kuwakamata ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
katika Mkutano huo mkaguzi wa polisi kata ya Riroda Luis Telemka amesema wamepokea maelekezo ya Mkuu wa wilaya kwa ajili ya utekelezaji wakati wowote kuanzia sasa ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi cha ulinzi shirikishi (Mgambo wenye mafunzo).