Site icon A24TV News

QURAN NI MUHIMU KATIKA MAISHA YETU-DK.MWINYI

Na Mosses Mashala .

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema ubora wa Quran ni muhimu katika maisha ya duniani na akhera.

Amesisitiza umuhimu wa Wazazi na Walezi kuhamasisha watoto na vijana kutekeleza mafundisho ya Quran kwa kuisoma na kuhifadhi.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika fainali za Mashindano ya 20 ya Kimataifa ya Quran Tajweed yaliyoandaliwa na Taasisi ya Khidmatulquran Islamic kwa kushirikisha nchi mbalimbali zikiwemo Msumbiji, Indonesia, Uturuki, Pakistan, Bangladesh, Misri, Comoro, Morocco, Afrika Kusini, Iran na Tanzania ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam tarehe 23 Machi 2024.

Aidha Rais Dk.Mwinyi amewataka Waalimu wanaofundisha Quran kwa njia ya Tajweed kuifikisha na kuisambaza Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi ametoa wito kuziunga mkono jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Khidmatulquran kwa kusimamia maadili na mienendo ya vijana kwa kuwapa ushirikiano katika kufikia malengo waliyojiwekea.

Mshindi wa kwanza wa Mashindano hayo ni Ilyaas Lamhayaoui wa Morocco aliyepata dola za kimarekani 5000, wa pili kutoka Misri dola za kimarekani 2500 na wa tatu kutoka Iran dola za kimarekani 1500.

Mwisho.