Site icon A24TV News

RAIS SAMIA ASIKIA KILIO CHA WACHIMBAJI WADOGO SONGWE, LESENI 37 ZA UCHIMBAJI MADINI ZATOLEWA

Na Mwandishi wa A24tv.

_Kunufaisha zaidi ya wachimbaji 5000

-Wamshukuru Rais Samia kwa kuwaendeleza wachimbaji wadogo

_Waziri Mavunde awataka wachimbaji kuongeza uzalishaji baada ya kupata Leseni

_Kwasasa wazalisha madini yenye thamani ya Bilioni 101 kwa miezi nane(8)

Serikali ya Awamu Sita, chini ya uongozi wa *Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan* imetekeleza ombi la siku nyingi la Wachimbaji w
Wadogo Wilayani Songwe kwa kuwatengea eneo la uchimbaji na kuwakabidhi jumla ya Leseni ndogo *37* zilizopo eneo la Kata ya Saza kutoka Leseni hodhi namba *RL0009/2014* ya iliyokuwa Kampuni ya Bafex Tanzania Limited.

Hayo yameelezwa leo Machi 23, 2024 na Waziri wa Madini, *Mhe. Anthony Mavunde* alipofika eneo la Saza Wilayani Songwe kukabidhi leseni 19 kwa wachimbaji wadogo wa Kikundi cha Songwe Gold Family (*SGF*) na wachimbaji wengine wadogo wadogo 18 huku mchakato wa kuendelea kutoa Leseni zaidi ukiendelea.

“Nimefika hapa leo kwa maelekezo ya *Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan*, ambaye amenielekeza nije kuwakabidhi leseni zenu za wachimbaji wadogo mlizomuomba na kuwa mnakwenda kuwekeza mitaji mikubwa sasa na kuongeza mzunguko wa fedha zitokanazo na shughuli za madini kufikia zaidi ya Trilioni moja,” amesema Mavunde.

Waziri Mavunde amesema pamoja na kwamba wachimbaji hao wanachimba kwa kubahatisha, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari, 2024 wamezalisha kilo 729.6 zenye thamani ya shilingi bilioni 101.06 na kueleza kuwa anaamini kwa kupatiwa leseni hizo hawatomwongusha Mhe. Rais kwa kuongeza uzalishaji na mapato yatokanayo na madini.

Pia, *Mhe. Mavunde* amebainisha kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inaondoa ujanja ujanja kwenye shughuli za uchimbaji madini ambapo tayari imekwishatangaza kufuta jumla ya leseni na maombi *2648* ambazo hazijaendelezwa na zimekiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini.

Mhe. Mavunde ameendelea kusisitiza kwamba hatasita kuendelea kufuta leseni kwa wamiliki wote ambao wanakiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini, ambapo ametoa mfano wa uwepo wa baadhi ya watu 6 tu wanaomiliki leseni zenye ukubwa wa zaidi ya ekari milioni 13.

Vilevile, Waziri Mavunde ameahidi kuwa baada ya Serikali kuwakabidhi wachimbaji wadogo Leseni ndogo za uchimbaji, inakwenda kuweka utaratibu mzuri wa kukabidhi taarifa za utafiti wa eneo hilo kwa kikundi cha SGF na hivyo kumuagiza Mkuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba leseni tatu namba 10, 11 na 12 ziwe wazi ndani ya siku 14 ili kupisha maeneo hayo kutangazwa ili kupata uwekezaji mkubwa.

Awali, akisoma risala kwa Waziri Mavunde, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wachimbaji wadogo cha Songwe Gold Family (SGF), *Bw.Simon Ndaki* amebainisha kwamba Kikundi chao kiliomba siku nyingi maeneo ya kuchimba na kupelekea kushindwa kuwekeza mitaji mikubwa kutokana na kukosa uhakika wa maeneo.

“Tunaahidi sasa kwamba tunakwenda kuwekeza mitaji mikubwa na kuhakikisha tunaongeza mchango zaidi wa mapato ya halmashauri na Pato la Taifa kwa ujumla,” amesema Ndaki.

Akieleza kuhusu masuala mbalimbali ya Wilaya ya Songwe, Mbunge wa Jimbo la Songwe, *Mhe. Philipo Mulugo* amwishukuru Serikali ya *Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan* kwa kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu na kumwomba Waziri Mavunde kupeleka shukrani za wachimbaji wadogo kwa Mhe. Rais na kueleza kwamba wapo tayari kusaidia kurejesha fedha zaidi ya *bilioni 72* zilizolipwa Bafex Tanzania Limited kwa uzalishaji mkubwa wa dhahabu.

Naye, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe, *Mhe. Solomon Itunda* ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya Wilaya yanatokana na shughuli za uchimbaji madini, na kuahidi kwamba ataendelea kushirikiana na wachimbaji wadogo kuhakikisha sekta ya madini inakua zaidi Wilayani Songwe.

 

Mwisho .