Site icon A24TV News

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUKEMEA UKATILI WA KIJINSIA.

Na John Walter-Manyara

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amewapongeza viongozi wa Dini nchini kwa juhudi zao za kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili na kuahidi kuwa,Serikali itaendelea kushirikiana nao vyema katika kuhakikisha vinatokomezwa katika maeneo yote nchini.

Twange ameyaeleza hayo leo machi 2,2024 mjini Babati alipomwakilisha mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa Bazara la Waislamu Tanzania (BAKWATA ) mkoa wa Manyara uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa Manyara.

Amesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi kuwa na hofu ya Mungu na hivyo kuepuka kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwamba wakitimiza wajibu huo ipasavyo watasaidia kutokomeza vitendo hivyo.

Aidha amewakumbusha wazazi na walezi kuwa makini katika malezi ya watoto wao hususani wa kiume ambao wamekuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na vitendo vya ulawiti akisema hapo awali nguvu kubwa ilielekezwa kwa watoto wa kike ambao walidhaniwa wako hatarini hivyo ni vyema uangalizi ukaelekezwa kwa watoto wa jinsia zote.

Sheikh wa Mkoa wa Manyara amesema amesema chanzo kikubwa cha vitendo vya ukatili wa kijinsia ni kukosekana kwa malezi bora katika jamii na kwamba BAKWATA wanaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kutoa elimu juu ya madhara yatokanayo na ukatili wa kijinsia ili kuinusuru jamii.