Site icon A24TV News

Wenyeviti wa vijiji na vitongoji watoa siku 30 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hai

Kwa ufupi:

Waliokuwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2019 wametoa siku 30 kwa halmashauri hiyo kuhakikisha wanalipa madeni ya posho zaidi ya Sh 200milioni wanazodai.

Hai.Waliokuwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro katika kipindi cha mwaka 2009 hadi 2019 wametoa siku 30 kwa halmashauri hiyo kuhakikisha wanalipa madeni ya posho zaidi ya Sh 200milioni wanazodai.

Wenyeviti hao ambapo ni zaidi ya 350 wanadai kutolipwa posho zao tangu mwaka 2010 hadi 2019 licha ya kupelekea malalamiko yao kwa maandishi katika ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari wakati walipokutana kwa dharura, mji wa Bomang’ombe, wilayani humo wamesema wamevumilia kwa muda mrefu kulipwa madeni yao na kwamba hawaoni chochote kinachoendelea.

Aizungumza Simon Mnyapanda ambaye alikuwa Mwenyekiti wa umoja wa Wenyeviti hao wilayani humo, amesema wametoa siku 30 sawa na mwezi mmoja ili waweze kulipwa stahiki zao

“Tunatoa siku 30 kulikuwa haki yetu, kwani tumefuatilia sana Kwa muda mrefu lakini tumeambulia kupata maelekezo ambayo hayatekelezeki,walisema watatupa fedha hizo junuari na hii ni March, hakuna kilichofanyika”amesema Mnyapanda ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Gezaulole Kwa wakati huo.

Mnyapanda ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Hai, amesema wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kudai kirafiki Kwa muda mrefu bila mafanikio na kila wakati huahidiwa bila utekelezaji wowote.

Aidha amesema baada ya siku hizo kukamilika kama Halmashauri itakuwa haijachukua hatua yeyote ikiwemo kuwaita na kukaa nao, watalazimika kutafuta mwanasheria kwa ajili ya kuishtaki Halmshauri hiyo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Nkuu Sinde kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi(CCM), Emily Swai amesema tangu ashike nafasi hiyo kwa vipindi vinne amelipwa posho mara mbili tu Kwa kukmbukumbu alizonazo na kwamba ni kitu ambacho kinawashangaza kwa kuwa walikuwa wanawatumikia wananchi kwa uzalendo.

“Tunatumika katika shughuli nyingi bila malipo, sasa hata hizi fedha ndogo ukisema ununue sukari imekwisha, wanashindwa kulipa ni aibu wakati wengine wakiwamo madiwani wanalipwa tena kwa wakati”amesema Swai

Emanuel Muro, aliyekuwa Katibu wa umoja huo wa Wenyeviti wilayani humo, amesema ni aibu kwa Halmashauri kushindwa kumlipa Mwenyekiti wa kijiji Sh 10,000 na wa kitogoji Sh 5,000 wakati walifanya kazi na kulitumikia taifa kwa uzalendo mkubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dionis Myinga amesema zipo jitihada ambazo zinafanywa na Serikali za kuwalipa wenyeviti hao madeni yao wanayodai zaidi ya Sh200 milioni.

“Kulikuwa na utaratibu wa zamani wa miaka ya 2010 mpaka 2015, kulikuwa na utaratibu wa ulipaji wa posho wenyeviti wa vitongoji, kadri muda ulivyosogea hadi mwaka 2015 ikaonekana halmashauri nyingine hazina uwezo wa kuwalipa hasa zile ambazo zina mapato kidogo, zile ambazo zikikutwa na mapato makubwa waliendelea kuwalipa”

“Serikali kuu ikaona jambo hilo sio jema kwa wale ambao halmashauri zao zina mapato madogo, hivyo serikali kuu ikawa inawalipa kutumia OC, wakaendelea kulipa yakatokea mabadiliko na utaratibu ukafutika, wakabaki wanaolipwa ni wenyeviti wa vijiji,”

“Mpaka wakati halmashauri ikiwa inawalipa hawa wenyeviti wa vitongoji na ikafika mahali serikali ikachukua mzigo huo ndio likawa hilo deni la zaidi ya Sh200 milioni, tulichokifanya tulihakiki deni kujiridhisha tukaweka utaratibu wa namna ya kuanza kulipa,”

“Serikali inafanya jitihada zote kuhakikisha wenyeviti hao wa vijiji na vitongoji wanalipwa, ambao tunawalipa sasahivi ni wenyeviti wa vijiji tu hao wa vitongoji utaratibu ulibadilika,”

 

Mwisho.