Na Mwandishi wa A24tv.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bahati Geuzye, amesema Baraza la Ushindani (FCT) litaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi katika masuala ya kiushindani na udhibiti wa Soko.
Ameyasema hayo Mei 3, 2024 Mkoani humo wakati akifungua semina ya elimu kwa wadau iliyoandaliwa FCT kwa Lengo la kutoa elimu kwa wadau kuhusu haki na wajibu wao ili kustawisha ushindani wa haki na kumlinda mlaji katika soko.
Akiwahutubia wadau hao wakiwemo
wawekezaji, watoa huduma, wafanyabiashara, na walaji/watumiaji na Taasisi za umma,
Geuzye amesema kuwa semina hii itasaidia wadau kuongeza kasi ya uwajibikaji katika soko na kutambua namna bora ya kutatua changamoto na migogoro ya kiushindani.
Naye Mkuu wa Idara ya Uchumi FCT, Bw. Kulwa Msogoti, ameongeza kuwa Baraza linahamasisha wadau wote wafanyabiashara, wawekezaji, watoa huduma, na walaji wawasilishe mashauri yao FCT iwapo hawajaridhika na maamuzi yanayotolewa na Tume ya Ushindani na Mamlaka za udhibiti kama vile EWURA, LATRA, PURA, TCAA, na TCRA.
Vilevile Afisa Sheria Mkuu wa FCT, Bi. Hasfa Said, amesisitiza kuwa FCT inatekeleza Sheria ya Ushindani ya Bunge na Kanuni za Baraza la Ushindani za mwaka 2012 na linaweza kutoa adhabu kwa wale wanaokiuka sheria hii, ikijumuisha faini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Chemba of Commerce Mkoa wa Mtwara, Bw Juma Napinda, amesema semina ya FCT imeleta mwamko wa wadau mbalimbali kujua wapi wanaweza kupata haki zao iwapo mlalamikaji anahisi hajatendewa haki, anaweza kukata rufaa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Bi Mwajuma Ankoni, amesema semina hii imewapa mwanga na elimu watakayoitumia siku za mbeleni na watakuwa mabalozi kwa wafanyabiashara ndani ya mkoa na nje ya mkoa.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Matakatifu Agotino (SAUT) Mtwara, Bw. Elia Charles, amesema semina hii ina manufaa na inampa uhalisia wa masuala ya biashara unaomsaidia kufundisha wanafunzi na itasaidia wafanyabiashara kuelewa namna ya ubora wa ushindani katikakufanya biashara bila kuathiri mlaji.
Mwisho