Site icon A24TV News

IGP Wambura awataka Maofisa wa Jeshi la Polisi kuzingatia weledi

Na Bahati Hai .

Mkuu wa jeshi la Polisi nchini,IGP Camilius Wambura amewataka askari na maofisa wajeshi hilo kufanya kazi kwa nidhamu,haki ,weledi na uadilifu ili kuleta tija kwa nchi bila kusahau kuwatendea haki wananchi.

Moshi.Mkuu wa jeshi la Polisi nchini,IGP Camilius Wambura amewataka askari na maofisa wajeshi hilo kufanya kazi kwa nidhamu,haki ,weledi na uadilifu ili kuleta tija kwa nchi bila kusahau kuwatendea haki wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 22,2024 katika hafla ya kuwatunuku nishani askari na maafisa 25 wa jeshi hilo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dk Samia Suluhu Hassan iliyofanyika Shule ya Polisi Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Wambura amewataka askari hao kuhakikisha nishani walizotunukiwa zinakuwa chachu ya utendaji wa kazi zao pia kuaamsha ari kwa wale ambao hawakubahatika kutunukiwa awamu hii ya kwanza lakini pia kuzingatia nidhamu,haki ,weledi na uadilifu ili kuleta tija kwa nchi yetu.

“Nishani hizi mlizotunukiwa ni vielelezo bora vya kupeleka kumbukumbu njema kwetu lakini pia kwa wengine wote ambao safari hii hawakubahatika kupata,hii ikawe chachu ya utendaji wa kazi kwenu wote mliotunukiwa lakini iende ikaamshe ari mpya kwa wale wengine wote ambao awamu hii hawakupata bahati”

“Twende tukazidishe tija na tukapambane,ni kazi ambazo ni lazima tuzitende na kuzingatia tunu zetu ambazo ni nidhamu haki weledi na uadilifu,twende tukazingatie hilo na huo ndio msingi wa jeshi la Polisi” amesema.

Pamoja na mambo mengine, amewataka Maofisa hao wa polisi kuhakikisha wanazuia uhalifu nchini ili taifa liendelee kuwa salama na lenye amani na kuwafanya wananchi waendelee na kazi zao za kiuchumi,siasa na za kijamii wakiwa na utulivu.

Naye, Mkuu wa Shule ya Polisi Moshi (CCP), Ramadhani Mungi amesema wataendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na weledi mkubwa.

Awali akizungumza Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Tixon Nzunda , amesema anaamini nishani hizo walizopewa watafanya kazi vizuri zaidi katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

“Naamini nishani hizi zitaimarisha utendaji ndani ya jeshi la polisi kufanya kazi vizuri zaidi kuhakikisha kwamba ndani ya jeshi la polisi Kuna nidhamu ya kutosha na hakuna rushwa na mkoa wa Kilimanjaro misingi ya haki inazingatiwa wakati wote” amesema Nzunda.

Mwisho