Site icon A24TV News

PPAA YAWEKA BAYANA MCHAKATO KUANDAA KANUNI ZA RUFAA UNUNUZI WA UMMA

Na Doreen Aloyce, Dodoma.

KAMISHNA wa Sera za ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha, Dkt.Frederick Mwakibinga amesema
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ipo katika mchakato wa kuandaa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024.

Dk,Mwakibinga amesema , kanuni hizo zitatoa wigo mpana wa kuwasilisha malalamiko ambapo mabadiliko hayo yatawapa wazabuni fursa ya kushindana kwa haki na uwazi katika zabuni mbalimbali.

Dkt.Frederick Mwakibinga ambaye amemuwakilisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Jenifa Omolo ameyasema hayo katika kikao kazi cha kupokea maoni ya uandaaji wa kanuni za Rufani za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024 kilichofanyoka jijini Dodoma.7

Aidha amesema kuwa kwa kuwa shughuli zote za ununuzi wa Umma zinafanyika kwa njia Kieletroniki kupitia mfumo wa NeST na kwa kuwa moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko yanayotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma nayo imekamilika katika mfumo wa NeST na inatarajiwa kuanza kutumika mwezi Julai 2024,

Ambapo ametoa rai kwa taasisi nunuzi, wajitahidi kutoa maoni yatakayowasaidia kuepukana na malamiko yasiyo na ulazima.

“Nina uhakika kupitia kikao hiki tutapata maoni na michango mizuri ambayo itaiwezesha Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma kupata Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 zinazoendana na wakati na zitakazoiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika ununuzi wa Umma”

“Nawapongeza PPAA Pamoja na Wizara ya Fedha na Ofisi ya Wanasheria Mkuu wa Serikali kwa kusimamia zoezi la uandaaji wa Kanuni hizi zitakazo iwezesha Serikali kutumia rasilimali zake kwa wakati, uwazi na haki”Amesema.

Aidha ameongeza kuwa anatambua wameshiriki Kikao kazi cha leo ili kuiwezesha Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kupokea maoni yatakayowezesha uandaaji wa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024. Hivyo, ni muhimu kuwasilisha kwa uwazi maoni yatakayowezesha uandaaji wa Rasimu ya Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ambapo
Tukio lililowakutanisha ni la muhimu kwa utendaji wa PPAA na Serikali kwa ujumla.

“Umuhimu huo unachagizwa na mabadiliko ambayo yanaendelea kufanyika katika sekta ya Ununuzi wa Umma nchini. Ambapo hivi karibuni, tumeshuhudia kutungwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na 10 ya mwaka 2023,sheria hii mpya ya Ununuzi wa Umma imeboresha masuala mbalimbali ikiwepo kupunguzwa kwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma,mfano, muda wa siku saba (7) za kazi kwa ajili ya kusubiri malalamiko ya wazabuni (cool off period) kabla ya kutoa tuzo umepunguzwa na kuwa siku tano (5) za kazi. Muda huo hautajumuisha njia za ununuzi ambazo hazihitaji ushindani kama vile single source, minor value procurement na shopping”

“Muda wa Afisa Masuuli kushughulikia malalamiko ya zabuni umepunguzwa kutoka siku saba (7) za kazi hadi siku tano (5) za kazi pale ambapo hataunda jopo. Endapo Afisa Masuuli ataunda jopo la mapitio ya malalamiko basi atakuwa na siku saba (7) za kazi na atatakiwa kuwajulisha washiriki wote wa zabuni juu ya uundwaji wa jopo hilo, sambamba na hilo muda wa PPAA kushughulikia malalamiko au rufaa umepunguzwa kutoka siku arobaini na tano (45) hadi siku arobaini (40)”Amesisitiza

“Ni imani yangu kuwa kupitia kikao kazi hiki maoni ya wataalamu wetu mliokusanyika hapa leo yatasaidia kupata kanuni bora zinazoendana na mazingira ya sasa”

Nae Katibu Mtendaji wa PPAA James Sando amesema Sheria na.10 ya ununuzi wa umma ilitungwa na kupitishwa na Bunge mwezi Septemba 2023 ambapo ili iweze kutumika kwa ufanisi ingetegemea kanuni za ununuzi ambazo zipo katika hatua mbalimbali na zitakamilika huku zikitarajia kuanza kutumia mwaka ujao wa fedha.

Aidha amesema sheria hizo zinaenda kupunguza changamoto kwenye Rufani za manunuzi zilizokuwepo ambazo zilikuwa zinalalamikiwa na wazabuni.

Wakiongea kwa nyakati tofauti washiriki wa kikao hicho kutoka taasisi mbalimbali wamesema kikao hicho kinaenda kuleta tija katika utendaji kazi.

Liipu Rweyemamu ni miongoni mwa washiriki hao ambaye ni Wakala wa huduma za Ununuzi Serikalini amesema kuwepo kwa utoaji wa maoni hayo itasaidia kuleta manufaa kwani sheria ya Sasa ina mabadiliko mengi ikiwemo kutumia muda mfupi katika kushughulikia malalamiko.

Ameiomba Serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa mawakala wa serikali jambo ambalo litasaidia kutoa huduma kwa ustawi zaidi.

Hata hivyo kikao hicho cha siku moja kinalengo la kuhakikisha kinawajengea uwezo maafsa hao kufanya kazi kwa uweledi nakwaa uharaka zaidi ili kuweza kutatua changamoto za Umma.

Mwisho