Doreen Aloyce, Zanzibar
Shangwe na Ndelemo vimetawala mara baada ya Maaskofu na waumini wa Dayosisi ya Zanzibar, kumpokea Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby alipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa Zanzibar.
Akiongoza jopo la Maaskofu na waumini wa waliotoka ndani na nje ya Dayosisi Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa amesema ujio wake ni wa faraja kubwa na furaha kwa wakristo kote nchini.
Aidha Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby amewasili nchini Tanzania kupitia Dayosisi ya Zanzibar, kwa lengo la kutembelea na kuona maeneo ya kihistoria mahali lilipo Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini Unguja yaliyotumika kufanya biashara haramu ya watumwa.
Pia Askofu Welby atapata fursa ya kuongoza Ibada kubwa itakayofanyika Kanisa kuu la Kristo Mkunazini Zanzibar.
Askofu Welby Mara baada ya kutembea na kupata historia ya maeneo hayo amesema amefarijika na kusikitishwa na ukatili uliofanyika na wakoloni kwenye soko la zamani la watumwa ambalo sasa ni Kanisa.
“Athari ya dhambi ni kubwa zaidi kuliko tunavyoweza kujua. Matokeo ya uovu wa utumwa ni zaidi ya ufahamu. Hii inaweza kusababisha watu kutazama mbali. Hata hivyo, ni lazima tukabiliane na maisha yetu ya zamani kwa uaminifu”.
“Hakika, ni pale tu tunapofanya hivyo, ndipo tunaweza kujua ukombozi kwa maana wokovu daima unahusisha kukiri kwetu, toba, na nia ya kuishi kulingana na Ufalme wa Mungu. Mungu aturehemu ili tutende haki, tupende rehema, na tuenende kwa unyenyekevu pamoja na Mungu wetu” alieleza Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby.
mwisho