Site icon A24TV News

ASKARI WA JESHI LA POLISI WA MKOA WA ARUSHA KUPITIA WALIOHITIMU MAFUNZO YA UDEREVA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA BARABARANI WAPEWA VYETI .

Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi

Askari wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha ambao wamehitimu mafunzo ya udereva leo Julai 12, 2024 wametakiwa kuzingatia mafunzo waliyopewa sambamba na kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani

Mkuu wa Operesheni za Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Salvas Makweli ambaye alimwakilisha Kamanda wa Polisi Mkoani humo ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya udereva yaliyoratibiwa na Jeshi la Polisi na kufanyika katika Chuo cha Ufundi Arusha.

ACP Makweli amebainisha kuwa Askari hao ambao wamefuzu mafunzo ya udereva wataenda kuwa msaada mkubwa hasa ikizingatia Jeshi hilo litapokea pikipiki na magari mengi hivi karibuni ambapo Askari hao watatumika kuendesha vyombo hivyo.

Aidha, amewataka kuhakikisha pindi watakapokua wanaendesha vyombo vya moto kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani na kujiepusha na udereva mbaya usiozingatia kanuni na sheria za usalama barabarani.

Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Profesa Mussa Chacha pamoja na kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kuamua kuwaruhusu maafisa wake kupata mafunzo hayo, amesema yataenda kuwa chachu kwa wananchi na jamii kwa ujumla ambapo wataona umuhimu wa kwenda kujifunza masuala ya usalama barabarani kwa kuiga mfano kwa Jeshi la Polisi.

Naye Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema Jeshi hilo limekua na utaratibu wa kutoa mafunzo ya udereva kwa makundi mbalimbali katika jamii, hivyo wakaona ni vyema kutoa mafunzo hayo kwa Askari wake katika kuwajengea uwezo lakini pia kufahamu sheria za usalama barabarani.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Magari katika Chuo hicho Mhandisi David Mtunguja amebainisha kuwa jumla ya madereva 179 wamehitimu mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa muda wa mwezi mmoja ambapo yalikutanisha madereva wa awali, madereva wanaongeza madaraja katika leseni zao na wale ambao walikua hawana vyeti vya udereva.

Konstebo wa Polisi Elizabeth Masai ambaye ni mnufaika wa mafunzo hayo, amebainisha kuwa kupitia mafunzo hayo yatamsaidia katika utendaji wake wa kazi hasa katika matukio ya dharura yanayohitaji madereva kwasababu ana uwezo na maarifa ya kuendesha vyombo vya moto.

Mwisho .