Site icon A24TV News

LISHE BORA MSINGI WA ELIMU BORA KWA WATOTO – DKT. MTAHABWA

Na Mwandishi wa A24tv.

Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 inasisitiza suala la upatikanaji wa huduma bora ya chakula na lishe kwa Wanafunzi Shuleni ili kuwaepusha kukatiza masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo njaa

Dkt. Lyabwene amesema hayo leo Julai 25, 2024 jijini Dodoma katika Kongamano la Kitaifa la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni, akisisiza kuwa kauli Mbiu ya Kongamano hilo inayosema *_Huduma ya chakula na lishe shuleni kwa afya na elimu bora_* inaakisi matakwa ya Sera ya Elimu na hivyo ni muhimu kuzingatia.

     Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa 

“Ili waweze kujifunza vizuri, Wanafunzi wetu wanahitaji mazingira bora na salama pamoja na kuwa na afya bora ya kimwili na kiakili” alisema Kamishna huyo.

Kamishna huyo amewaeleza Wadau wa Kongamano hilo kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Mpango wa Shule Salama na kwamba katika Mpango huo suala la lishe Shuleni ni la muhimu na linazingatiwa.

“Ni kweli Wizara inatoa Sera, nyaraka na miongozo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa afua za kielimu. Lakini utekelezaji wa nyaraka hizo muhimu unategemea sana ushiriki wa Wadau wote”. alibianisha Dkt. Mtahabwa.

Akizungumza katika Kongamano hilo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Ernest Hinju ameahidi kufanyia kazi maoni ya Wadau na kushirikiana nao katika kusimamia na kushauri suala la chakula kwa shule za bweni na kutwa ili kuimarisha ujifunzaji.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Mradi Pamoja Tuwalishe Bi. Vick Macha amesema mradi huo wa miaka 5 unatekelezwa kwenye shule 367 kwa mkoa wa Mara na Dodoma, na unalenga kuwafikia Wanafunzi 316,000.

Mwakilishi kutoka Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bi. Debora Esso amesema Shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kushauri juu ya utoaji wa chakula na lishe shuleni.

Mwisho.