Site icon A24TV News

MAMLAKA YA MAPATO TRA YAZIDI KUJIDHATITI UKUSANYAJI MAPATO NCHINI.

Na Richard Mrusha

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023/2024 imeweza kukusanya shilingi trilioni 27 .64 nakuipa fursa Serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo na kustawisha maisha ya watanzania pasipo na wasiwasi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai Mosi, 2024 na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, imesema makusanyo yameongezeka kwa asilimia 14.50 yakilinganishwa na makusanyo ya Sh trillioni 24.14 ya mwaka wa fedha 2022/2023.

 

“Kiasi cha fedha tulichokusanya ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.67 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 28.30,” nakubainisha kuwa katika kipindi cha robo mwaka ya nne, kwa maana Aprili hadi Juni, 2024 Mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya Sh trillioni 7.09 sawa na ufanisi wa asilimia 99.46 ya lengo la kukusanya kiasi cha Sh trillioni 7.15.

Katika taarifa hiyo, Kidata anasema kuna ongezeko la makusanyo kwa asilimia 24 yakilinganishwa na Sh trillioni 5.72 ya makusanyo yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Hata hivyo taarifa hiyo inaeleza kuwa makusanyo ya mwaka 2023/24 yameongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini na shughuli za viwandani.

Pia amesema vitendo vya ukwepaji kodi na kutozingatia sheria za mamlaka hiyo, vimeendelea kushamiri miongoni mwa makundi mbalimbali ya walipa kodi wakiwamo watu binafsi, kampuni za ndani na za Kimataifa.

Pamoja na changamoto hiyo, taarifa ya Kidata imehimiza ulipaji kodi kwa kufuata sheria zilizopo na utekelezaji wake kuzingatia misingi ya utawala bora.

Mwisho .