Site icon A24TV News

MANYONI YAJIPANGA UTATUZI CHANGAMOTO YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

Na Mwandiahi wa A24rv .

Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ni miongoni mwa Halmashauri za Wilaya 91 nchini zinazokabiliwa na migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu, ambapo imekuwa ikipata madhara mbalimbali ikiwemo uharibifu wa mashamba hekari mia mbili themanini katika vijiji kumi na nne na watu wawili kupoteza maisha katika kipindi cha mwaka 2023-2024..

Hayo yamebainika na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Leila Sawe ambaye pia ni Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya utatuzi wa migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu yaliyoendeshwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ikihusisha taasisi zake za TAWIRI, TAWA, TFS na wadau wa UNDP.

Sawe amewataka Viongozi wa Vijiji na wananchi kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ya siku tatu kwa nadharia na vitendo na kuwa mabalozi wazuri kutoa elimu hiyo kwa wanachi wengine

” niwasihi tuache utamaduni wa mazoea ya kuhudhuria mafunzo bila kuyafanyia kazi” amehimiza Sawe

Naye, mwakilishi wa Mkurugenzi wa wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na utalii Antonia Raphael amesema kuwa, migongano baina ya binadamu na wanyamapori ni changamoto katika uhifadhi na katika kuitatua Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mkakati wa kuzuia changamoto hiyo ambapo utoaji mafunzo kwa wananchi ni kipengela kimojawapo kati ya vipengele saba vya mkakati huo.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Manyoni Bw.Jummanne Makanda ametoa wito kwa wananchi kutumia mafunzo hayo ili kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii nchini

” babu zetu walihifadhi rasilimali hii ya wanyamapori ndio maana leo tunanufaika na mapato ya Utalii na kujivunia fahari ya kuwa na wanyama hawa, hivyo nasi hatuna budi kuwahifadhi ” amehimiza Makanda.

Kwa niaba ya Wananchi wa Manyoni, Diwani wa Kata ya Mjini Mhe. Saimon Mapunda ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuwezesha mafunzo ya utatuzi wa migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waaribifu ikiwa ni mwitikio wa kilio cha wananchi cha madhara yanayosababishwa na wanayamapori hususani Tembo.

Aidha, Mafunzo ya utatuzi wa migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu ambayo yanatolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake za TAWIRI, TAWA, TFS pamoja na wadau wa UNDP yanaendelea kwa siku tatu ambapo baada ya wananchi kupata mafunzo kwa nadharia wapo uwandani kwa mafunzo ya
Vitendo.

Mwisho .