Site icon A24TV News

SELF WAJA NA HUDUMA YA BIMA KULINDA MALI

Na Richard Mrusha

Mfuko wa SELF ulio chini ya Wizara ya Fedha umeanzisha huduma mpya ya bima kwa lengo la kulinda mali za wateja.

Akizungumza Julai Mosi,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Afisa Bima katika Mfuko wa SELF, Rasuli Sadala, amesema huduma hiyo imeanzishwa kuwawezesha wateja waishi kwa amani hasa yanapotokea majanga mbalimbali

“Kuna majanga mbalimbali yanatokea mfano ya wizi, moto, ajali mbalimbali na yanakuja bila mtu kuwa amejiandaa, lakini ukiwa na bima inaweza ikakulinda kulingana na majanga.

Kwahiyo Mfuko wa Self umekuwa wakala kwa ajili ya kutoa huduma hizi kwa wateja wetu.


“Endapo gari lako likipata ajali, kuungua moto au kuibiwa, kampuni ya bima itakufidia kukurudishia. Kuna bima za moto kwa ajili ya kulinda sehemu ya biashara, nyumba na bima za wizi ambazo zinalinda mali yako na bidhaa ambazo ziko kwenye maduka kwahiyo tunatakiwa tuishi kwa kujiamini,” amesema Sadala.

Aidha amesema wana matawi 12 yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini ambako elimu ya fedha na bima inatolewa.

Mfuko huo pia unatoa mikopo ya biashara na kilimo kwa taasisi na mtu mmoja mmoja yaani wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi kwa ajili ya kuboresha makazi.

Amesema pia wanaendelea kuboresha mikopo ya vikundi ili kuwafikia wateja wa chini kwa lemngo la kuwainua Watanzania.


Sadala amewataka Watanzania kutembelea maonesho hayo katika banda la Wizara ya Fedha ambako wanapatikana ili kupata elimu ya fedha, huduma ya bima na mikopo.

Mwisho.