Site icon A24TV News

SERIKALI YATAKIWA KUONDOA VIKWAZO VYA KIBIASHARA KWA VIJANA

Na Geofrey Steven

Serikali kupitia maafisa maendeleo ya jamii na biashara wametakiwa kuondoa vikwazo vya kibiashara vya kusafirisha mazao mikoani na nje ya nchi kwa vijana waliojitokeza kujiajiri kupitia shughuli za kilimo.

Rai hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Eliakimu Mnzava wakati alipotembelea na kukagua mradi wa uwezeshaji vijana Kiuchumi kupitia Kikundi cha Vijana cha Agri – Genius.

Mradi huo wenye thamani ya shillings milioni 32 Uliowezeshwa kupitia mkopo uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Vijana, wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na mazao cha mbogamboga na matunda.

“Nawaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Biashara kuwasaidia vijana wanaojiajiri katika shughuli za kilimo kwa kuondolewa vikwazo pale wanaposafirisha mazao yao ndani na nje ya nchi” alisema Kiongozi huyo na kuongeza;

“Nikiongelea vikwazo naamaanisha wapewe sapoti ya halii ya juu, Kama kuna vibali wanahitaji wapewe mapema ili waweze kufanya shughuli zao kwa urahisi na biashara zao ziweze kuwa za kimataifa na kupiga hatua zaidi kiuchumi, maana hii itawezesha wengibe kuiga na kupunguza wimbi la vijana tegemezi” alisema.

Mnzava alisema kuwa ameridhishwa  na shughuli zinazofanywa na vijana hao wazalendo wa kulitumikia Taifa lao na kuwataka kuongeza juhudi katika kazi zao na kuwa mfano na vijana wengine ambao bado hawaoni fursa zinazotengenezwa na serikali.

“Taifa letu linawategemea vijana wabunifu na wapambanaji katika kusukuma gurudumu la maendeleo mbele, nyie ni vijana wa mfano, kazi mnazozifanya wahimizeni na vijana wenzenu kufanyakazi hasa za kujiajiri na kuajiri wengine” Amesema Mnzava.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mwenyekiti wa Kikundi cha Agri – Genius, Godfrey Rogath, ameishukuru Serikali kwa kuweka mkakati imara wa kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kutoa mikopo ambayo inawapa fursa vijana kujiajiri na kujiinua kiuchumi.

“Mkopo huu umetuwezesha kuongeza mtaji wetu kutoka shilingi milioni 2 na kufikia shilingi milioni 32 mpaka sasa na hii ni  baada ya kupata mkopo wa shilingi  milioni 30 kutoka ofisi ya Waziri Mkuu” alisema mwenyekiti huyo.

Amesema kuwa wameweza kujenga kitalu, nyumba na kuongeza eneo la kilimo kutoka heka 1 na kufikia Heka 4 wanayomiliki sasa.

Ameongeza kuwa Mkopo huo mbali na kuwawezesha wao kujipatia kipato lakini pia vijana wengi wameweza kujiajiri na kuwa mfano kwa vijanza wenzao wanaokuja kujifunza shughuli za kilimo.

Awali kikundi hicho chenye wanachama watano kilianza mwaka 2022 na kusajiliwa kwa namba ARU/ ARU/VIJ/2022/20247.

 

Mwisho