Site icon A24TV News

VIJANA WAASWA KUACHA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA KUEPUKA UTEGEMEZI KATIKA FAMILIA.

Na Geofrey Stephen Arusha .

Vijana katika kata ya Sekei Jijini Arusha wameaswa kuacha matumizi ya dawa za kulevya kwani zinasababisha nguvu kazi ya taifa kupotea, kuwafanya kuwa tegemezi katika familia zao pamoja na kupata madhara mbalimbali ya kiafya.

Mkaguzi Kata ya Sekei Jijini Arusha, Mkaguzi wa Polisi (A/INSP) Ditrick Mtuka ametoa wito huo leo Julai 05, 2024 wakati akizungumza na Waraibu wa Dawa za kulevya wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha.

“Vijana mnapaswa kujiepusha na makundi yanayoweza kusababisha kutofikia ndoto zenu kwani makundi hayo yanaweza kusababisha kutumbukia kwenye matumizi ya dawa za kulevya”. Alisisitiza Mkaguzi huyo.

Sambamba na hilo amewataka vijana hao kuhamasisha vijana wengine walioathirika na dawa za kulevya kufika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu ili kujikwamua katika wimbi hilo lakini pia kutoa taarifa za baadhi ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo ili hatua zichukuliwe dhidi yao.

Pia amewataka kwenda kuanzisha miradi midogo midogo kama kilimo cha mbogamboga na biashara ndogo ndogo kuliko kwenda kukaa vijiweni ambako wanakutana na ushawishi wa matumizi ya dawa hizo za kulevya.

Halikadhalika A/INSP Mtuka amesema ili kuwanusuru na janga hilo, jamii haina budi kuungana kuwasaidia vijana kwa kuwapa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya kama ambavyo Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kwa kuwaweka karibu na kuwapatia elimu ya kujitambua.

Mwisho .