Wafanyabiashara katika soko kuu la Arusha wameiomba halmashauri ya jiji la Arusha kuboresha miundo mbinu ya soko hilo kutokana na majengo yake kuchakaa na maduka kuvuja wakati wa mvua na kusababisha kukosa mvuto kwa wateja wakiwemo watalii wanaofika kwa ajili ya kujipatia mahitaji mbalimbali.

Miongoni wa kero walizozitaja   ni pamoja na uchakavu wa soko hilo, baadhi ya maeneo kukosa umeme,ukosevu wa vyoo,watu kujisaidia ovyo kwenye vizimba vya biashara,sehemu ya maduka kuvuja wakati wa mvua,Wafanyabiashara kuacha vizimba na kupanga bidhaa zao kiholela ,jambo linalosabahisha wateja walikimbie soko hilo na kwenda masoko mengine.

 

Wakiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika sokoni hapo,wafanyabiashara hao wameziomba mamlaka za usafiri kuruhusu magari madogo ya usafiri aina ya haice kushusha na kupakia kando ya soko hilo ili kuwarahisishia Wateja wao wa mbogamboga wanaofika kununua bidhaa hizo kupata usafiri, tofauti na sasa ambapo wanunuzi hao wamelazimika kukimbilia masoko mengine ya Samunge na Kilombero ambako kuna usafiri wa karibu

Baadhi ya  wafanyabiashara hao,Turuneshi Hasan(Chuda),Heleni Macha na Gladness Temba walisema kero hizo zimekuwa za muda mrefu na hakuna jitihada zozote 

 zinazochukuliwa na serikali licha ya malalamiko yao kuyatoa mara kwa mara kwa wahusika.

 

“Tumekuwa tukilalamika kwa muda mrefu kuwa soko hili halina miundo mbinu bora ikiwemo ya vyoo ,umeme,watu kufanyabiashara bila mpangilio,ukosefu wa ofisi ya viongozi wa soko, kukojoa ovyo na vinyesi kwenye vizimba, maduka kuvuja kutokana na uchakavu ,hali hii imesabajisha wateja wengi kuhamia masoko mengine,tunaomba serikali ifanyie matengenezo kero hizo”


Akijibu Kero hizo mkuu wa soko hilo,John Haule alisema serikali kupitia halmashauri ya jiji la Arusha ,imejipanga kuwajengea mazingira wezeshi ya biashara ikiwemo kulifanyia matengenezo soko hilo.

Aidha aliwapongeza wafanyabiashara hao kwa kuendelea kulipa kodi ya serikaki kwa ufasaha na kusisitiza kwamba kero zote walizozitoa zinafanyiwa kazi na muda mrefu zotapatiwa ufumbuzi.

 

“Niwashukuru sana wafanyabiashara waliotoa kero zao na sisi kama viongozi wenu tutahakikisha zinafanyiwa kazi kwa wakati ikiwemo ujenzi wa ofisi ya wafanyabiashara ila niwasisitize endeleeni kulipa kodi kwa maslahi mapana ya taifa lenu”

 

 

 

Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Inyasi  Mallya alisisitiza kuwa mambo mengi yanashindwa  kufanyika katika soko hilo kutokana na ukosefu wa ofisi ya wafanyabiashara. 

Hata hivyo alitoa siku 14 kwa wafanyabiashara walioondoka kwenye vizimba vyao na kufanya biashara kiholela wahalikishe wanarejea kwenye vizimba  walivyopangiwa haraka iwezekanavyo.

Aidha alisema wafanyabiashara wanaotoa lugha za matusi na wanaojisaidia ovyo katika vizimba vya soko hilo na kusababisha adha ya uchafu kali watakabiliwa na faini ya sh, elfu 50 papo hapo.

 

“Kero kubwa inayotukabili hapa ni pamoja na miundo mbinu mibovu  ya soko kuu ikiwemo ukosefu wa vyoo eneo la bondeni, tunachoshauri kwa uongozi wa halmashauri soko hili ni bora likafumuliwa na kujengwa upya na likiachwa hivi biashara zitakufa”

 

 

 

Diwani wa kata ya kati ,Abdul Tojo aliwatoa hofu wafanyabiashara hao kwa kuwaleleza kwamba suala la uboreshaji wa soko hilo upo katika hatua za mwisho na muda sio mrefu ujenzi wake utafanyika ikiwemo ujenzi wa gorofa kwani soko hilo limepitwa na wakati.

 

“Niwaombe wafanyabiashara shirikianeni na viongozi wenu kutatua kero ndogo ndogo ila suala la maboresho ya soko hilo lipo mbinoni kujengwa gorofa, kwani soko hili limezeeka limejengwa enzi za zamani”

Mwisho .