Site icon A24TV News

Wanawake wanaochipukia kwenye nafasi mbalimbali za uongozi watakiwa kuwa na udhubutu .

Happy Lazaro,Arusha .

Wanawake wanaochipukia kwenye nafasi mbalimbali za uongozi wametakiwa kuwa na udhubutu wa kugombea nafasi mbalimbali na kuwa mstari wa mbele katika kutoa maono kwani wana mchango mk.ubwa katika jamii .

Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mbunge wa bunge la Afrika Mshariki ,Fatuma Ndangiza wakati akizungumza katika mdahalo wa kwanza wa Afrika Mashariki kuhusu wanawake kwa maswala ya uongozi bora .

Aidha mdahalo huo uliwashirikisha wanawake wanaochipukia kwenye nafasi mbalimbali za uongozi na kufanyika katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki.

Fatuma amesema kuwa,lengo la mdahalo huo ni kuwakutanisha vijana hao wanaochipukia kwenye uongozi kuweza kubadilishana uzoefu na viongozi mbalimbali wanawake waliohudhuria pamoja na wabunge wanawake na kuweza kufikia ndoto zao.

Ameongeza kuwa,wanataka kuona wanawake wanakuwa na udhubutu mkubwa katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki katika jamii inayowazunguka .

Fatuma amefafanua kuwa,kupitia mdahalo huo wataweza kusikia sauti na mchango wa wanawake hao wanaochipukia katika uongozi na kuweza kupata uzoefu mbalimbali namna wengine walivyoweza hata kufanikiwa kuwa viongozi wakubwa kwenye nafasi mbalimbali .

“Mdahalo huu ni wa kwanza kufanyika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo tumewashirikisha wanawake zaidi ya mia moja kutoka nchi zote za jumuiya ya Afrika Mashariki na tutakuwa tunafanya kila mwaka kwani vijana wana shauku kubwa ya kujifunza maswala mbalimbali ya uongozi. “amesema .

Aidha mdahalo huo umeandaliwa na Umoja wa wanawake wa bunge la Afrika Mashariki kwa kushirikiana na chuo cha maendeleo ya jamii Tengeru na sekretariti ya jumuiya ya Afrika Mashariki .

Baadhi ya washiriki katika mdahalo huo,Mhadhiri msaidizi kutoka chuo cha TICD,Sia Machange amesema kuwa mdahalo una manufaa makubwa sana kwani umewashirikisha viongozi wakubwa wanawake pamoja na viongozi chipukizi wanawake na kuweza kujadili maeneo ya uongozi katika kuangalia changamoto wanayokabiliana nazo wanawake ili waweze kufikia malengo yao hasa katika maswala ya uongozi .

“Ni jukumu letu kuwashauri viongozi vijana kwa kuwashirikisha katika programu ya uongozi wa vijana na kubadilishana uzoefu na viongozi kizazi chipukizi ” amesema.

Amesema kuwa ,Wanawake vijana wanapaswa kutumia ujuzi wao uliopo hasa kuokoa baadhi ya wanawake ambao wanakabiliwa na changamoto katika uongozi pamoja na maeneo mengine.

Kwa upande wake Msimamizi wa kiongozi wa wanawake vijana ,Caren Massawe ambaye pia ni mwanasheria amebainisha changamoto na vikwazo zinachowakwamisha wanawake kuwa ni fikra potofu za kijinsia na upendeleo, mitazamo ya kitamaduni na kijamii katika uongozi kuwa ni upendeleo wa kiume dhidi ya wanawake.

“Viongozi vijana wa kike wanatatizwa na changamoto nyingi katika kupata na kutekeleza majukumu ya uongozi ikiwa ni pamoja na kukosa watu wa kuigwa na washauri kutokana na kuwatisha viongozi wa kike.”amesema .

Massawe ameongeza kuwa kiongozi wa vijana wa kike anatakiwa kutambua fursa na fursa kuu ambazo wanawake wanazo katika kuleta mabadiliko na ubunifu katika
Karne ya 21 pamoja na kuleta uzoefu wao wa kipekee na utofauti katika majukumu mbalimbali ya uongozi.

“kama tunavyojua wakati viongozi wanawake wanashawishi uundaji wa sera na utetezi katika ngazi ya kitaifa ya kimataifa” amesema Massawe.

Mwisho