Site icon A24TV News

ZAIDI YA WATU MIA SITA WAMEPATA HUDUMA YA UPIMAJI AFYA YA MOYO BURE JKCI

Na Richard Mrusha

Dkt Jakaya Kikwete atembelea Banda la JKCI akijionea watanzania wakipatiwa huduma afya ya moyo bure katika maonyesho ya Sabasaba

RAIS Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ametembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kujionea jinsi ambavyo watanzania wakipatiwa huduma ya upimaji na ushauri kuhusu afya ya moyo bure katika viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mheshimiwa Rais Mstaafu kutembelea banda hilo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano JKCI, Anna Nkinda, amesema kuwa zaidi ya watu 600 wamepatiwa huduma ya upimaji na ushauri kuhusu afya ya moyo bure toka kuanza kwa Maonesho ya Kimataifa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tarehe 28 juni.

“Tunatoa shukrani zetu za dhati kabisa kwa mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, kwani juhudi zake ndizo zimepelekea leo hii watanzania wengi wanapata uduma hizi bobevu hapa hapa nchini katika Taasisi yetu ya JKCI,” alisema Mkuu huyo wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano JKCI

Aliongeza, “Vile vile nachukua fursa hii kuweza kuwakaribisha watu wote kutoka sehemu mbali mbali ya nchi yetu kuja katika maonesho haya na kutembela banda letu la JKCI ili kuweza kupatiwa huduma na ushauri kuhusu matibabu ya moyo.

Na kwa upande wake Betrice Mmari kutoka Kampuni ya Telehealth amesema kuwa wameingia katika makubaliano na JKCI ili kuwawezesha watu wote wanaoitaji matibabu na ushauri kwa njia ya mtandao (online) ambapo mgonjwa ataweza kuweka ahadi ya kuonana na daktari na kuweza kutibiwa akiwa popote pale ndani ya nchi ama nje ya nchi.

Beatrice amesema kuwa katika huduma hii ya online, mgonjwa anaweza kuchagua dakari ambaye atapenda kutibiwa naye na atapangiwa tarehe ya kuonana naye kwa mtandao ama uso kwa uso.

Naye, DKT .Elias Birao ambaye ni mmmoja wa madaktari wa JKCI ambaye naye anatoa huduma za afya ya moyo na ushauri katika banda hilo amesema kuwa wamepokea watu kutoka mikoa karibu yote ya Tanzania ambao wamefika kupata huduma na ushauri kuhusiana na magonjwa ya moyo na presha.

Amesema kuwa wamebaini kuwa watu wengi nchini wamekuwa wakitembea na magonjwa ya moyo na presha bila wao wenyewe kujua, hivyo ametoa wito kwa watanzania kuwa na tabia ya kufanya vipimo mara kwa mara ili kulinda afya zao.

Mwisho