Site icon A24TV News

RAIS MWINYI: CHINA IMESAIDIA SANA ZANZIBAR

Na Mosses Mashala .

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema China imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika mambo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya hospitali.

Rais Dk. Mwinyi Amesifu ukarabati mkubwa wa Hospitali ya Abdalla Mzee Pemba, utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta ya afya, msaada wa vifaa vya matibabu na dawa, pamoja na udhamini wa masomo kwa madaktari wazalendo

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 26 Agosti 2024, Ikulu Zanzibar, alipozungumza na timu ya madaktari 29 kutoka kundi la 33, walioongozwa na Kaimu Balozi Mdogo wa China Zanzibar, Chang Ming, chini ya kiongozi wa madaktari hao, Dk. Yuzheng Huang, waliofika kumuaga baada ya kufanya kazi nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Aidha, Dk. Mwinyi ameishukuru Serikali ya China kwa ushirikiano wake na Zanzibar kupitia sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo sekta ya afya, unaochangiwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina Zanzibar na China tangu kuasisiwa kwake.

Halikadhalika, Dk. Mwinyi amesema kuwa mbali na misaada hiyo, China pia imeisaidia Zanzibar kwa kutoa msaada wa kitaalamu katika udhibiti na kinga za maradhi mbalimbali, ikiwemo kichocho kwa Unguja na Pemba, pamoja na kuleta teknolojia mpya ya uchunguzi wa maradhi ya kansa.

Naye kiongozi wa timu ya madaktari hao, Dk. Yuzheng Huang, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na uongozi wa Wizara ya Afya kwa ushirikiano waliowaonesha tangu walipofika Zanzibar mwezi Septemba mwaka 2023, pamoja na kusifia ukarimu wa watu wa Zanzibar.

Mwisho .