Site icon A24TV News

WAKULIMA WAFUGAJI KATENI BIMA

Na Richard Mrusha Dodoma

WAKULIMA na wafugaji wameaswa kukata bima ya mazao na mifugo yao ili kujilinda dhidi ya majanga yanayoweza kujitokeza kwa mifugo kufa au mazao kukumbwa na ukame.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la NIC kwenye maonesho ya wakulima na wafugaji (88) Afisa Bima wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Experius Nchanila amesema katika msimu huu wa maonesho hayo ,NIC wamekuja na bima mbalimbali ikiwemo bima mkakati za kilimo na ufugaji ambazo zinalenga kumkwamua mkulima dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri mifugo au mazao yake.

Amesema kwa mkulima kukata bima ya mazao na mifugo yake itamsaidia kufidiwa pindi majanga yanapojitokeza na kufanya uharibifu na hivyo kumwezesha kuendelea na shughuli zake bila kikwazo chochote.

Nchanila amesema ,vitu kama moto,kimbunga,ukame,wadudu waharibifu na mvua za mawe zinaweza kuleta uharibifu wa mazao ya mkulima hivyo bila kuwa na bima ni dhahiri mkulima ataathirika na hivyo kupata hasara.

“NIC imeona kilimo ni sekta nyeti kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa ,hivyo tumeona tuilinde sekta hiyo ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta hiyo.” Amesema Nchanila

Kwa upande wa bima ya mifugo amesema bima hiyo inatolewa kwa mifugo kama ng’ombe,mbuzi, kuku ,nguruwe ili kumwezesha mkulima kufabya ufugaji wenye tija ambapo mfugaji akipata majanga ya mifugo yake anafidiwa pia.

“Mfugaji anapata bima ya mifugo inapokufa kwa ajali,kufa wakati wa kuzaa ,mfugo kuchinjwa kwa maelekezo ya kitaalam kwamba hawezi kupona tena kama alikuwa na magonjwa yasiyotibika.” Amesisitiza

Nchanila amesema,tangu NIC imeanza kutoa bima za wakulima na wafugaji mwitikio umekuwa ni mkubwa huku akiendelea kuwasisitiza wananchi kufika katika banda hilo kwa ajili ya kupata elimu kuhusu shughuli za bima.