Site icon A24TV News

RASMI SASA VIJIJI, VITONGOJI VYA TARAFA YA NGORONGORO KUSHIRIKI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA 2024.

Na Geofrey Stephen Arusha .

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametangaza kuwa jumla ya Vijiji 12, 333, mitaa 4,269 na Vitongoji 64, 274 vitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Akizungumza Jijini Arusha mapema  leo Jumatatu Septemba 16, 2024 kwenye Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,

Mhe. Waziri  Mchengerwa amewaambia wanahabari kuwa kwenye orodha hiyo kumejumuishwa maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa tangazo la serikali ambayo pia yalihusisha Tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha.

“Matangazo haya yanajumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa Tangazo la serikali namba 673 na 674 ambayo yalihusisha pia Tarafa ya Ngorongoro. Lengo la hatua hii ni kuhakilisha kuwa maeneo haya yanapata uwakilishi mzuri kiutawala pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi zinazowiana na mahitaji ya wananchi.” Amesema Mhe. Waziri.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo katika kuunda serikali ya wananchi kidemokrasia ikiwa ni pamoja na kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la mpigakura kwa mustakabali wa maendeleo na kuendeleza juhudi za serikali katika kujitafutia maendeleo endelevu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Mohamed Bayo alisema wamepokea kwa furaha tamko la waziri kuunganisha vijiji 65 vilivyokuwa vimefutwa Ngorongoro.

“Tumepokea kwa furaha sana tamko la Serikali kurejesha vijiji 65 na vitongoji 242 vilivyokusa vimefutwa kurejeshwa na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa”

Mwisho.