Na Joseph Ngilisho ARUSHA
JUMLA ya Walimu wakuu wa shule za msingi wapatao 9132 katika mikoa 13 nchini wamepatiwa mafunzo ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule yaliyolenga kuwajengea ujuzi na maarifa ili kufikia viwango bora vya elimu kwa kuboresha utendaji wao wa kazi.
Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya ADEM ,Dkt Leonard Akwilapo wakati akifunga mafunzo ya siku tatu katika halmashauri ya Arusha,kwa awamu ya tatu kwa walimu wakuu 1398 wa mikoa ya Arusha na Manyara yaliyoandaliwa na wakala wa maendeleo ya uongozi wa Elimu ADEM na kufadhiliwa na benki kuu ya dunia chini ya mpango wa mradi wa BOOST.
Dkt Akwilapo alisema kuwa mafunzo ya aina hiyo yamekuwa yakitolewa katika mikoa mbalimbali hapa nchini na kwamba katika awamu ya kwanza na ya pili walimu wakuu wapatao 9132 wamenufaika na mafunzo hayo na kukamilisha mikoa yote nchini
“Ni wazi kwamba ili ulete mageuzi chanya lazima uanze na safi ya uongozi na nyinyi mliopo mbele yangu ndio viongozi naamini mafunzo hayo yataenda kuleta utofauti katika shule zenu kwani hakuna kazi yoyote inaweza kuleta ufanisi bila kuwa na mafunzo”
“Katika awanu zote mbili na hii ya tatu ambayo tunahitinisha leo walimu wakuu wa shule za msingi wamepatiwa mafunzo ya uongozi ,usimamizi na utawala wa shule”.
Mwenyekiti huyo wa bodi alisisitiza kuwa walimu wakuu hao wa shule ,mafunzo hayo yazingatie uendelezaji wa ofisi,ukusanyaji wa Takwimu ,uandaaji wa mipango ya maendeleo ya shule, motisha kwa walimu,usimamizi wa rasilimali watu,fedha ,usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji ,ustawi na usalama wa wanafunzi ,ufuatiaji na usimamizi wa ufanisi wa shule, usimamizi wa ujenzi shuleni na ushirikishwaji wa jamii katika maendeleo ya shule.
Awali Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt Maulid Maulid alisema kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yamelenga kuwajengea uwezo wakuu wa shule waweze kusimamia ipasavyo usimamizi wa taaluma pamoja na miradi ya maendeleo ya shule ili kuleta ufanisi wa kiutendaji shuleni.
Alisema mafunzo hayo yamefanyika katika mikoa mbalimbali hapa nchini na awamu hiyo ya tatu yamefanyika katika mikoa ya Arusha na Manyara yakilenga kuleta tija, ufanisi na matokeo chanya mashuleni.
Dkt Maulid alitoa rai kwa walimu wakuu waliopata mafunzo hayo kuhakikisha mafunzo hayo yanaleta mabadiliko kwa walimu wanaowaongoza ,kamati za shule ilu maarifa hayo yalete mabadiliko kwa jumuiya nzima ya shule.
Alimpongeaza rais Samia Suluhu Hasani kwa kuleta mapinduzi katika sekta ya elimu ya kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mindombuni na kutoa fedha za mafunzo ambazo hapo awali hali hiyo haikuwepo.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo wakala wa elimu Maendeleo ya Uongozi wa Elimu EDEM,Ombeni Mbwilo alisema mafunzo hayo yameshirikisha washiriki kutoka halmashauri 14,halmashauri saba kutoka Arusha na Halmashauri saba kutoka mkoa wa Manyara.
Alifafanua kwamba washiriki kutoka mkoa wa Arusha walikuwa 594 sawa na asilimia 100 na washiriki 666 sawa na asilimia 100 walitoka mkoa wa Manyara.
“Kwa ujumla walimu wakuu 1260 walipatiwa mafunzo hayo katika awamu hii ya tatu na kwa halmashauri ya Arusha jumla ya walimu wakuu walikuwa 102 sawa na asilina 100 walihudhulia mafunzo hayo wakiwemo 41 wanawake”
Ends…