UJENZI WA UWANJA WA MPIRA WA SAMIA SULUHU HASSAN ARUSHA WAFIKIA PAZURI!
Ngirisho1
Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa Mpira wa Miguu Mkoani Arusha wa Samia Suluhu Hassan unaojengwa na kampuni ya China ya Railway Construction Engineering Company Limited (CRCEB)kutoka nchini China unaendelea vizuri na upo asilimia nane tangia kuanza kwa mradi huo Julai mwaka huu.
Akiongea na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo jana, msimamizi wa shughuli za ujenzi, Denice Mtemi alisema kuwa shughuli za Ujenzi mradi huo wenye thamani ya sh,bilioni 286.9 zinaendelea vizuri na hakuna changamoto kubwa.
Alisema kwa sasa wapo katika hatua ya awali ya kuchimba msingi ambayo imefikia asilimia 95 na wanaendelea kumwaga zege jembamba kwa ajili ya kupokea zege kubwa la kubeba uwanja .
“Mradi umeanza mwezi wa saba na kinachoendelea kwa sasa ni hatua ya awali ya kuunganisha kazi za msingi ambazo zimefikia asilimia 95 na kinachoendelea kwa sasa ni kumwaga zege jembemba ili kupokea zege kubwa kwa ajili ya kusapoti jengo zima la uwanja”
“Hatua ya kimradi hadi sasa ipo asilimia nane ikiwa tayari tumeshafanya ikiwa tumeshafanya muunganiko kwa asilimia zaidi ya 80 kwa maana ya ofisi pamoja na marazi ya timu ya mkandarasi pamoja na timu ya washauri wa serikali “Alisema.
Mtemi ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kitaalamu kwa maandarasi ,alisema kazi ya kumwaga zege jembamba inatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili zijazo ili waanze kumwaga zege kubwa kwa ajili ya Msingi wa Jengo.
Alisema hadi sasa hakuna changamoto yoyote kubwa iliyojitokeza itakayowafanya wacheleweshe mradi na wanatarajia kukamilisha mradi huo ndani ya wakati kwa awamu ya kwanza julai 2026.
Alisema changamoto ya maji iliyokuwepo hayo hapo awali kwa sasa imetatuliwa baada ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (AUWSA) kukubali kuwapelekea bomba la maji linalojitegemea kutoka tenki kubwa lililopo eneo la jirani.
“Mwanzo tulikuwa tunapata maji kidogo ya bomba tukigawana na wanakijiji ila kwa sasa Auwsa wamekubali kutupatia maji yanayojitegemea kutoka kituo chao cha maji kilichopo eneo la jirani hivyo hatutakuwa na changamoto hiyo”
Alisema hadi sasa wameajiri wafanyakazi zaidi ya 380 wakiwemo mafundi na madereva na wanatarajia kadri shughuli zitakavyokuwa zikiendelea watakuwa na wafanyakazi wasiopungua 3000 .
“Kutokana na mkataba tunatakiwa kukamilisha mradi kabla ya julai 2026 lakini tumezungumza na wizara pamoja na mshauri elekezi kuona jinsi gani tunaweza kupunguza muda huo na mpango upo tayari unaandaliwa kuhakikisha mradi unakamikika awamu ya kwanza 2026 ili serikali ipate muda wa kuutumia na kuona mapungufu kabla ya mashindano ya AFCON kutimua vumbi”
Uwanja huo unaojengwa katika kata ya Olmoti jijini Arusha ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuingiza watu wapatao 32,000 na niwakisasa na bora zaidi katika nchi za Afika Mashariki kwani pamoja na mambo mengine ,utakuwa na vyumba vya watu mashuhuri kwa pande mbili za uwanja na pia utatumika kwa michezo ya Riadha .
Tanzania ni mwenyeji wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON)ifikapo mwaka 2027 ikiwa ni juhudi za rais Samia.