Site icon A24TV News

WASHIRIKI ELFU MOJA KUSHIRIKI MBIO ZA DYSLEXIA AWARENESS RUN OKTOBA 20 MWAKA HUU

Mwandishi wetu ,Arusha .

Arusha .Washiriki Elfu moja wanatarajiwa kushiriki katika mbio za “Dyslexia Awareness Run” zinazotarajiwa kufanyika oktoba 20 mwaka huu katika uwanja wa mgambo mkoani (karibu na Gymkhana) Arusha .

Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Dyslexia Tanzania , Caudence Ayoti ambao ndio waandaaji wa mbio hizo .

Amesema kuwa, lengo la mbio hizo ni kusambaza uelewa kuhusiana na Dyslexia kwani Taasisi hiyo inajihusisha na kusambaza uelewa kuhusu changamoto za kujifunza kwa watoto.

“Dyslexia ni changamoto ambayo inampata mtoto katika kujifunza ,kuandika, kusoma na kuhesabu ambapo mbio hizo zitasaidia taasisi hiyo kuendelea kusambaza uelewa kuhusiana na changamoto hiyo kwenye jamii”.amesema Ayoti.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Dyslexia Tanzania , Caudence Ayoti akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mbio hizo

Ayoti ameongeza kuwa ,washiriki hao watakimbia mbio za kilometa 5 na 10 ambapo washiriki kwenye mbio hizo watapata medali za kipekee kutoka Shanga Foundation ambazo zinatengenezwa na walemavu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaunga mkono pia.

Aidha amesema kuwa,kiingilio katika mbio hizo ni shs 35,000 ambapo ametoa wito kwa wananchi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ili waweze kuiunga taasisi hiyo mkono katika kuendelea kusaidia watoto wenye changamoto hiyo.

Kwa upande wake Meneja Rasilimali watu kutoka Shanga Foundation ambao ndio wamefadhili medali hizo,Janet Steven amesema kuwa,Taasisi hiyo ya kijamii inashughulika na watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakitengeneza medali hizo wa lengo la kujipatia kipato.

Amesema kuwa, taasisi hiyo imechukua uamuzi wa kufadhili mbio hizo kwa lengo la kuwasaidia walemavu hao na pia kusambaza uelewa kuwa wanaweza ili waweze kuungwa mkono kwani medali hizo ndio wametengeneza wenyewe.

Kw upande wake Mwenyekiti chama cha riadha mkoa wa Arusha ,Gerald Babu ameipongeza taasisi hiyo kwa kuanzisha mbio hizo ambazo zinalenga kutatua changamoto hiyo ya Dyslexia kwa watoto kwani ni jambo zuri sana na ni mfano wa kuigwa na jamii.

Babu ametoa wito kwa wadau na jamii mbalimbali kujitokeza kwa wingi katika mbio hizo kwa lengo la kuwaunga mkono kwa ajili ya kusaidia jitihada hizo .

Mwisho.