Site icon A24TV News

DKT. NDUGULILE AMETUACHIA SIMANZI KUBWA“ – DKT. TULIA

Na Dorin Aloyce

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kifo cha Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile, kimeacha simanzi kubwa kwa Bunge na Watanzania kwa ujumla kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mtaa wa Uzunguni A, Jijini Mbeya leo tarehe 27 Novemba, 2024, Dkt. Tulia amesema kuwa nyota ya Dkt. Ndugulile imezimika wakati akiwa ameanza kung’ara katika anga za kimataifa. Alikuwa aanze rasmi majukumu yake mapya ya kimataifa mwezi Machi mwaka 2025

 

Dkt. Tulia amesema kuwa Bunge limepoteza Mbunge mahiri ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI. Mchango wake uliwezesha kufanikisha mabadiliko makubwa ya sheria na sera katika sekta za afya na mapambano dhidi ya UKIMWI.

Aidha, amewataka Wananchi wa Kigamboni kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho wamempoteza Mbunge wao na kumuombea apumzike kwa amani.

Dkt. Ndugulile amefarikidunia usiku wa kuamkia leo nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.