Taarifa hii fupi kwa umma inakuja baada ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
(THRDC) kufanya ziara mwezi Novemba 2024 katika Tarafa ya Ngorongoro, Wilayani
Ngorongoro. Lengo kuu la ziara ilikuwa ni kuangalia hatua zilizochukuwa na Serikali katika
kutatua changamoto zilizoainishwa katika ripoti ya watetezi wa haki za binadamu ya mwaka 2023
iliyoonyesha kuzorota kwa huduma za kijamii katika Tarafa ya Ngorongoro Wilayani Ngorongoro
mkoani Arusha pamoja na agizo la Mhe Rais Samia Suluhu Hassan la kurejeshwa kwa huduma
aliyoitoa mwezi September 2024 baada ya maadamano ya wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro.
Katika ziara hii, tulitembelea baadhi ya maeneo na kuangalia maeneo ya huduma hizi, na pia
wananchi walipata nafasi ya kutoa maoni yao, viongozi wa jamii, watetezi wa jamii pamoja na
viongozi wa serikali kutoka Halmashauri ya Wilaya na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (The Ngorongoro Conservation Area (NCA) ni mojawapo ya
hifadhi huru inayojitegemea hapa nchini. Hifadhi hii haipo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya
Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kuwa ina sheria yake iliyoianzisha ya Mwaka 1959. (The
Ngorongoro Conservation Act). Eneo hili linasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(Ngorongoro Conservarion Area Authority, NCAA). NCAAni mamlaka iliyoundwa na sheria yake
mwaka 1959 kwa lengo la kusimamia eneo hili maalum lenye malengo matatu katika uanzishwaji
wake, yaani: kulinda maslahi ya wenyeji, uhifadhi na utalii.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo la kipekee lenye matumizi ya mseto ya ardhi. Sheria ya
NCA inatambua eneo hili kwa ajili ya uhifadhi, utalii lakini pia kwa matumizi ya watu hasa jamii
ya wamasai ambao ni wengi na makabila mengine kama wahadzabe na wabarbaig ambao sheria
imewataja.1 Eneo hili linatumika pia kwa shughuli za kifugaji na shughuli mbalimbali za kimila.
Asimia kubwa ni msitu , pia kuna uoto wa asili wa nyanda za juu kaskazini lenye kuchukua asilimia
20 za NCA, pia milima ipo mingi na maeneo mengineyo ni tambarare na mabonde kama mabonde
5 ya kreta.
1 Kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
Page 2 of 8
2.0 Marejeo ya Changamoto zilizoainishwa kwenye ripoti ya Watetezi kuhusu huduma
Baadhi ya changamoto za huduma za jamii zilizokuwa zinaibuliwa na wananchi mara kwa mara
na pia zilizoainishwa kwenye ripoti ya mwaka 2023 ya watetezi wa haki ni:
- a) Kufifishwa kwa Huduma za Msingi za Jamii
Moja ya changamoto kubwa wakati wa zoezi la kuhamisha watu toka mwaka 2022 ilikuwa ni
kuzorotesha na kuweka vikwazo kwa huduma za kijamii kwa wananchi wanaobaki kama mkakati
wa kuweka mazingira ya wananchi kulazimika kuhamia katika kijiji cha Msomera na kwingine.
Huduma mbabalimbali za jamii kama vile huduma za mabweni kwa shule za msingi na sekondari,
huduma za vyoo mashuleni, huduma za afya , huduma za barabara, huduma za maji , vibali vya
ujenzi n.k. Mfano-
- Kuhamishwa kwa fedha za huduma za Kijamii- Takriban billion 4 ya fedha za
huduma za kijamii ziliozopangwa Kwenda tarafa ya Ngorongoro toka mwaka 2021
hadi 2024 zilirudishwa na kupelekwa kwingine. Mfano, Kiasi cha shilingi za
kitanzania, 355,500,000 cha fedha za mradi wa uviko-19 (Covid-19 relief funds)
zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika tarafa ya
Ngorongoro zilihamishiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni bila
kuazimiwa na baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
- Kukosekana kwa mabweni, madarasa na matundu ya vyoo Mashuleni.
Wanafunzi katika shule zote Ngorongoro walikuwa na uhaba mkubwa wa
madarasa, mabweni pamoja vyoo. Hali hiyo iliwalazimu wanafunzi kulala zaidi
ya wawili kwenye kitanda kimoja kutokana na upungufu wa mabweni. Kwa mfano
shule ya msingi Enduleni pekee yenye wafanauzi 1600 ilikuwa na upungufu wa
matundu 42 ya vyoo.
- Kuzorota kwa huduma za afya na kuzuiwa kwa Huduma ya Afya ya Dharula.
Huduma za afya zilizorota sana katika tarafa ya Ngorongoro ambapo huduma ya
dharua pamoja na chanjo kupitia mradi wa Flying Medical Service ulioko chini ya
Kanisa Katoliki ilisitishwa mnamo 08/04/2022. Vilevile huduma za kukosa
majengo mapya , kuzuiwa kwa ndege kuruka, kuondolewa kwa fedha za miradi,
kunyimwa vibali vya ujenzi,ukarabati n.k.
- Wananchi kukatiwa huduma ya maji na NCAA. Wananchi walikatiwa huduma
ya maji na hivyo kukosa huduma ya maji. Vilevile maji kwaajili ya mifugo
hawakuwa nayo baada ya kuzuiwa Kwenda kunywesha mifugo yao katika bondo
la Ngorongoro mwaka 2016.
- Changamoto ya Barabara. Wakazi wa tarafa ya Ngorongoro hawana Barabara
zinazopitika kwa urahisi hasa za kwenda kwenye makazi yao, lakini kwenye
maeneo ambayo mahoteli ya kitalii yanajengwa Ngorongoro wananchi
wameshuhudia barabara zikitengenezwa.
- b) Kuzuiwa kwa mikutano ya kijamii, kimila na kisiasa
Page 3 of 8
Kulikuwa na jitihada za kuzuia shughuli zozote za kimila katika Tarafa ya Ngorongoro Wilayani
Ngorongoro. Taarifa za uwepo wa mikakati hii ilianza kubainika pale shughuli ya kimila za
kumsimika Mbunge wa Ngorongoro kuwa kiongozi wa kimila ilipogubikwa na changamoto ya
watu kuzuiwa kutoka maeneo mengine ya Wilaya na nje ya Wilaya kushiriki tukio hilo. Shughuli
hizi za kuwasimika viongozi wa kimila zimekuwa zikifanyika miaka yote na katika maeneo yote
walipo jamii hii ya Kimasai.
Kwa mfano Mwezi Juni mwaka 2024 sherehe ya kimila iliyokuwa imepangwa kumsimika mtetezi
wa haki za jamii hiyo Wakili Joseph Oleshangai zilizuiliwa kwa amri ya Polisi. Barua hiyo ya
Polisi ya terehe 14/3/2024 inaeleza kuzuia kusanyiko lolote katika kata zote za Tarafa ya
Ngorongoro.
- c) Vikwazo vya kiiuchumi
Wakazi wa tarafa ya Ngorongoro walizuiwa kwenda kuuza mifugo yao katika minada mbalimbali
hasa kwa wakazi wa tarafa ya Ngorongoro. Vikwazo hivi vya kiuchumi vimefanya wananchi hawa
wazidi kuwa katika mazingira magumu ya kubudu kuendesha yao.
- d) Kunyimwa Vibali vya Ujenzi
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ilisitisha vibali vya kufanya ujenzi au ukarabati wa aina
yoyote wa nyumba za wananchi na taasisi zinazotoa huduma za jamii. Kwa mfano ukarabati wa
hospital, shule za msingi, nyumba za watumishi n.k. Kwa mfano shule ya msingi Endulen vyoo
vilikuwa vimejaa na iliwalazimu wanafunzi kujisaidia nje au porini. Hapohapo shule ya Enduleni,
wanafunzi walikuwa wanalala 4 kwenye kitanda kimoja kutokana na ujenzi wa mabweni uliokuwa
unaendelea kusitishwa. Mwaka 2023 Shule ilikuwa na jumla ya wanafunzi 1,900 (wakike 785 na
wa kiume 1054) ina mabweni mawili tu. Kati ya hao wanafunzi 617 wanaishi bweni (wakike 272
na wa kiume ni 345) na kulikuwa na mabweni mawili tu.
- e) Gharama ya kupaki gari (Parking fee) kwa wakazi wa tarafa ya Ngorongoro
Wakazi wa tarafa ya Ngorongoro wanakumbana na changamoto ya kulipia gharama ya kupaki gari
ndani ya makazi yao. Mtu yeyote anayemiliki gari na ni mkazi wa tarafa ya Ngorongoro alitakiwa
kulipa kiasi cha Tshs. 118,000 kwa gari binafsi na Tshs 300,000 kwa gari ya biashara kwa mwaka.
Mbali na gharama ya kupaki gari, ilikuwa ikifika 10:30 jioni kama mtu hajaingia getini
hakuruhusiwa tena kuingia hata kama mtu huyo ni mkazi wa Ngorongoro.
- f) Kukosekana kwa uhuru wa Habari na Watetezi wa Haki za Binadamu
Ripoti ya mwaka 2023 ilibaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kujieleza na
pia uhuru wa vyombo vya habari kutoa taarifa juu ya hali ilivyokuwa Ngorongoro.
Watetezi wa haki za binadamu pamoja na mashirika ya utetezi wa haki za wafugaji walikuwa
katika wakati mgumu sana kufanya kazi zao za utetezi kipindi chote cha zoezi hilo. Baadhi ya
watetezi wa jamii walijikuta wakikimbia nchi kunusuru maisha yao huku wengine
wakiunganishwa katika kesi ya mauaji yao. Kutokana na uwekezaji huo kjiji kilikuwa kinapata
faida ya shilingi milioni 240 hadi 250 kwa mwaka.
Page 4 of 8
- g) Jaribio la Kuzuia washiriki chaguzi za mwaka 2024 na 2025 na Kufutwa kwa Vijiji
Tarehe 3 Agosti 2024, baadhi ya viongozi na wakazi wa Ngorongoro walifanya mkutano na
waandishi wa habari, wakidai kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imehamisha majina
ya wapiga kura kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, eneo ambalo ni asilimia 2 tu ya wakazi wa
Ngorongoro wamehamia. Tamko hilo lilitolewa baada ya Serikali kufuta kata 11 na vijiji 25 katika
tarafa hiyo kupitia Tangazo la Serikali Na. 673 la Agosti 2, 2024. Kupitia tangazo hilo wakazi wa
tarafa ya Ngorongoro zaidi ya 100,000 wasingeweza kuchagua viongozi katika uchaguzi wa
mwaka 2024/2025.
3.0 Maandamano ya Wananchi na Maagizo ya Rais Samia
Jumapili, Agosti 18, 2024, mamia ya wanajamii wa Kimasai wanaume, wanawake, na vijana
waliandamana kupinga kunyimwa huduma za msingi, ubaguzi, na haki ya kuishi katika ardhi ya
Ngorongoro, mahali ambapo ni makazi yao ya asili. Waandamanaji walibeba mabango yenye
jumbe mbalimbali yenye kuonyesha hisia zao na maandamano hayo yalidumu takribani wiki moja.
kichocheo kikubwa cha maandamano ya Agosti 2024 ilikuwa ni madai ya wakazi hawa
kupokonywa haki yao ya kupiga kura ndani ya Ngorongoro pamoja na huduma za kijamii.
Kufuatia maandamano hayo, tarehe 23 Agosti 2024 Mhe. Willium Lukuvi, Waziri wa nchi, ofisi
ya waziri mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) aliambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa
Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula, Mkuu wa Mkoa
wa Arusha Paul Makonda na Kamishna wa Operesheni na mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh
Juma Haji. Mhe alipeleka ujumbe wa Rais Samia kwa wananchi hawa waliokuwa katika siku ya
tano ya Mgomo.
William Lukuvi aliwaeleza kuwa Rais Samia ameagiza kurejeshwa kwa huduma za kijamii,
kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na kuondolewa vikwazo vyote
vilivyowekwa kwa wakazi wa tarafa ya Ngorongoro.
Agizo hilo la Mhe. Raisi lilikuja baada ya wakazi wa tarafa ya Ngorongoro kufanya maandamano
ya takribani wiki moja baada ya mabadiliko ya kiutawala yaliyoondoa hadhi ya kiutawala ya Kata
ya Ngorongoro, na kuathiri wakazi zaidi ya 110,000 kwa kufuta vijiji 25 na kata 11 katika tarafa
hiyo kupitia Tangazo la Serikali Na. 673 la Agosti 2, 2024, ambapo endapo tangazo hilo
lisingefutwa basi wakazi wa tarafa ya Ngorongoro wasingeweza kuchagua viongozi katika
uchaguzi wa mwaka 2024/2025.
Tangazo hilo lilionyesha kuwa vituo vyote vya kupiga kura katika Kata ya Ngorongoro
viliondolewa kwenye daftari rasmi, na usajili wa wapiga kura wengi ulionekana kuhamishiwa
Handeni mkoani Tanga. Endapo mabadiliko hayo kupitia tangazo hilo yasingetenguliwa
yangewanyima wakazi wa tarafa ya Ngorongoro haki yao ya msingi ya kupiga kura katika
uchaguzi wa 2024 na 2025 kinyume na ibara ya 5(1) na 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
4.0 Hali ya Huduma za Kijamii Miezi Miwili baada ya Agizo la Rais Samia
Page 5 of 8
Awali ya yote, tunapenda kutumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mhe Rais Samia Suluhu
Hassan kwa hatua nzuri aliyoichukua ya kutuma wajumbe wake wakati wananchi wa Tarafa ya
Ngorongoro wakiwa katika maandamano yaliyodumu kwa siku tano. Uamuzi huo wa kutuma
watu wa kusikiliza vilio vya wananchi na kuagiza vilioo vyao vifanyiwe kazi vimeonyesha busara
na hekima ya Mhe Rais. Kwa muda mrefu watetezi wa haki za binadamu tumekuwa tukishauri
uongozi wa juu wa nchi ukutane na wananchi, na mara baada ya Mhe Rais kutuma wajumbe wake
tumeanza kuona faida ya hatua hii kwa wananchi wa Tarafa hii. Pamoja na kwamba serikali ndio
imelalamikiwa kusababisha changamoto hizi, kitendo cha Mhe Rais kuamua vikwazo hivi
viondelewe imeleta matumaini mapya kwa watu wa Ngorongoro, kimetufurahisha sisi watetezi wa
haki za binadamu na pia hatua hii inalinda taswira ya nchi katika eneo la haki za binadamu na
utawala bora.
Baada ya kufanya ziara mwaka 2024 katika Tarafa ya Ngorongoro, Mtandao wa Watetezi wa Haki
za Binadamu Tanzania (THRDC) umejionea hali ya haki za binadamu pamoja na huduma za
kijamii katika tarafa ya Ngorongoro. Tunatambua na kuthamini juhudi za hivi karibuni
zilizofanywa na Serikali kurejesha huduma muhimu za kijamii katika Tarafa ya Ngorongoro, eneo
ambalo liliathiriwa kwa kiasi kikubwa na kusitishwa kwa huduma hizi kwa takriban mwaka
mzima. Kusitishwa kwa huduma hizo hasa kuanzia mwaka 2022 kuliathiri jamii za asili na
wafugaji katika eneo hilo ambalo ni mseto.
Taarfa ya Ngorongoro yenye idadi ya watu 100,000 ina jumla ya kata 11, Vijiji 25, Shule za Msingi
22, Shule za Secondary 3, Hosptali Moja ya Mission na Vituo vya Afya na Zahanati 13. Vyote
hivi vimekuwa na changamoto nyingi za kuwahudumia wannchi kwa miaka minne sasa.
Pamoja na kwamba bado ukarabati wa maeneo mengi ya huduma za kijamii haujaanza.
Tumejionea mikakati na hatua za awali za urejeshwaji wa huduma za msingi kama huduma za
afya, elimu, na miundombinu ya msingi. Haya yanaelezwa zaidi kama ifuatavyo;
- Hamlshauri iliunda kamati maalum ya kwenda kuzunguka katika tarafa ya Ngorongoro
kwa lengo la kutambua mahitaji ya awali ya haraka katika kufanyia kazi maagizo ya Mh
Rais ya kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro.
- Utengaji wa Bajeti – Kuna bajeti iliyotengwa kwa miradi kadhaa ya maendeleo katika
Tarafa hiyo ya Ngorongoro, ikiwemo shule, miundombinu, hospitali, n.k. Kwa mfano,
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Bw. Benezeti Bonipace, alitangaza kuwa
Halmashauri imetenga takribani shilingi bilioni 2 za kitanzania kwa miradi ya maendeleo
katika eneo hilo. Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji na Diwani wa Kata ya
Alaileai, Mhe Shutuk Kitamwas pia aliieleza kuwa baadhi ya miradi imeanza kutekelezwa,
na miradi mingine imependekezwa kusubiri hadi mwishoni mwa mwaka kwa sababu za
usalama, ikiwemo ukarabati wa shule. Viongozi wengine wakiwemo wenyeviti wa vijiji
na madiwani waliofikiwa na ziara hii , nao wameonyesha kutambua uwepo wa budget hii
inayotengwa kwa ajili ya ukarabati wa maeneo ya huduma za kijamii. Mfano, katika jumla
Page 6 of 8
ya budget billion 2 iliyotengwa kwa ajili ya kuboresha huduma, baadhi ya vijiji vifuatavyo
vimeweza tengewa pesa kiasi kifuatacho;
- Kwa eneo la shule ya msingi ya Ndian zimetengwa jumla gharama za shilling za
kitanzania milioni mia moja kumi na moja, laki tano na elfu kumi na mia tano hamsini (Tsh
111,513,550). Gharama hizi zikiwa zinajumuisha maboresho na umaliziaji wa nyumba za
watumishi wawili, ukarabati wa madarasa nane na pamoja na ukarabati wa matundu kumi
na mbili ya vyoo.
- Shule ya msingi ya Endulen imetengewa jumla ya gharama za shiling za kitanzania milioni
mia tatu arobaini na sita, laki tis ana elfu moja mia sita tu (Tsh346,901,600). Gharama hizi
zikiwa zinajumuisha maboresho na ukarabati wa madarasa tisa,umaliziaji wa mabweni
matano na ukarabati wa matundu kumi na mbili ya vyoo.
- Shule ya sekondari ya wasichana Ngorongoro zimetengewa jumla ya gharama za shiling
za kitanzania milioni mia moja na nane, laki sab ana elfu Hamsini mia tisa na ishirini na
tano tu (Tsh 108,750,925). Gharama hizi zikiwa zinajumuisha umaliziaji wa bweni la
wanafunzi themanini (80), umaliziaji wa jengo la maabara ya kemia na ukarabati wa
matundu kumi na mbili ya vyoo.
- Shule ya sekondari ya Nainokanoka zimetengwa jumla ya gharama za shiling za kitanzania
milioni mia mbili kumi na nane, laki mbili na elfu sitini na nane n amia mbili na ishirini tu
(Tsh 218,268,220). Gharama hizi zikiwa ni ukarabati wa mabweni matatu, umaliziaji wa
bwalo la chakula na ukarabati wa matundu kumi na mbili ya vyoo.
- Kituo cha afya cha Osinon zimetengwa jumla ya gharama za shiling za kitanzania milioni
mia moja na tisini na nane,laki tano na elfu sabini na saba na ishirini na tano tu (Tsh
198,577,025). Gharama hizi zikiwa zinajumuisha ukarabati wa kliniki ya mama na mtoto,
chumba cha upasuaji na huduma za matibabu za wagonja wa kawaida.
- Demokrasia na Uchaguzi – Kuhusu wapiga kura waliosajiliwa, Tarafa ya Ngorongoro
inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura waliosajiliwa kwa
uchaguzi wa 2024/2025. Hii inaonyesha kuwa kuna wananchi wa Tanzania katika eneo
hilo, na ni vyema kwao kutumia haki yao ya kidemokrasia. Pamoja na hayo, wana
Ngorongoro sasa wanahisi kuwa na uhuru wao na uwepo wa viongozi wao wa serikali
baada ya muda mrefu. Walieleza kuwa hata wanaona viongozi wakitembelea eneo hilo na
kushughulikia shida zao, jambo ambalo ni faraja kubwa baada ya miaka michache iliyopita
ambapo walionekana kama wahamiaji katika nchi yao. Wananchi wameeleza kuwa
wameshiriki vizuri zoezi la uchaguzi katika hatua za awali.
- Huduma ya Elimu pia imefanyiwa kwa hatua kidogo, ila bado mengi yanatakiwa
kufanyika. Kwa sasa, kuna mifuko ya simenti tayari imewekwa kwenye baadhi ya shule,
tayari kwa kuanza ujenzi. Ilielezewa ya kwamba, ujenzi wa maeneo ya shule yatatumia
muda mwingi, na hayawezi kufanyika pindi wanafunzi wapo madarasi. Hivyo itegemewe
kuanza punde tu likizo zitakapoanza. Mfano Mwenyekiti wa Kijiji cha Ndian, alileza kuwa
Page 7 of 8
walikubaliana na Mkuu wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya , wasubiri kwanza Watoto
wafunge shule ndipo zoezi la ukarabati wa shule uanze.
- NCAA imepiga hatua kama kuondoa tozo za magari kwa wakazi, ambazo sasa hutozwa
mara moja kwa mwaka badala ya kila siku, na kuendelea kutoa huduma muhimu pale
inapowezekana.Muda wa kuingia eneo la tarafa ya Ngorongoro sasa umeongezwa kutika
saa 10.30 hadi mwisho wa kuingia kuwa saa 12.30 jioni.
- Huduma za Afya pia zimeendelea kama kawaida. Halmashauri ya Ngorongoro imeendelea
kutenga bajeti na pia kutoa nguvu kazi kwa hospitali ya Enduleni kama ilivyopangwa. Hii
imewapa moyo sana wana Ngorongoro. Viongozi wa Parokia ya Enduleni wa Kanisa
katoliki wanaosimamia Hosptali ya Enduleni , nao wamesema wameanza kuaona
mabadilko na ushirikiano na serikali toka agizo la Rais Samia kufanyiwa kazi. Ingawa bado
swala la vibali vya ujenzi wa majengo mapya wameeleza kuwa bado ni changamoto. Pia
bado ndege ya huduma za dharura ( Fyling Medical Doctor) haijaruhusiwa kuendelea na
huduma zake.
- Wananchi na viongozi pia wameeleza kulalamikia ukamataji wa watu wanaojenga majengo
ya kawaida yasiyohitaji vibali kwa mujibu wa sheria ya Hifadhi. Wapo baadhi ya watu
ambao wameshapelekwa mahakamani wakiwa wanafaya ujenzi na ukarabati wa nyumba
zao za kawaida na za asili.
- Mamlaka ya Hifadhi ya Nngorongoro, kupitia Afisa Habari Mwandamizi wa NCA ndugu
Kassim Nyaki, aliezea kuwa NCA kwa sasa inaendelea kutekeleza yale mambo ya msingi
yaliyopo mikononi mwao kama kusomesha wanananzi , kuboresha miundo mbinu nk. Hata
hivyo swala la ada kwa wananfuzi wa Ngoronngoro limeendelea kulalamikiwa na
wananchi kuwa bado linachangamoto nyingi kwa kuwa wanafunzi wengi hawapati
huduma hii kama inavyotakiwa. NCA wamesitiza kuwa wanatoa huduma hii kulingana na
budget wanatengewa ukizingatia kuwa kwa sasa fedha zote za makusanyo hazipo tena
chini ya usimamizi wa Hifadhi kama ilivyokuwa awali.
- Wananchi na Viongozi pia walihoji kwanini ahadi ya kuonana na Mhe Raisi Samia,
iliyotolewa na viongozi aliowatuma inachukua muda mwingi kukamilika. Wamesisitiza
kuwa ni muhimu kwa ahadi hii ikafanyiwa kazi ili kutoa nafasi ya Mhe Raisi kukutana na
kujadiliana na wananchi wa Ngorongoro kuhusu changamoto zote katika eneo hili la
Ngorongoro na Lolioondo. Wamesititiza , mkutano huu uwe maalum kwa jamii ya
wanangorongoro bila kuwachanganya na watu toka wilaya zingine za zenye jamii ya
kimasai kwa tatizo lao halifanani na maeneo mengine.
THRDC inasisitiza umuhimu wa kuzingatia ustawi wa jamii, haki za binadamu sambamba na
juhudi za uhifadhi na kulinda ikolojia, kwani vyote vinaweza kuendelezwa kwa faida ya watu na
mazingira.
5.0 Wito Wetu
- a) Licha ya yote haya, tunamshauri Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kutimiza ahadi yake ya kutembelea Tarafa ya Ngorongoro ili
Page 8 of 8
kuwasikiliza wananchi na kupata uelewa kamili wa changamoto wanazokabiliana nazo.
Ombi hili liliibuka wakati wa maandamano ya amani yaliyofanyika Ngorongoro Agosti
mwaka huu 2024, ambapo kilio cha wananchi kilikuwa ni kumwomba Rais afike
Ngorongoro ili asikilize changamoto zao na kusaidia kuzitatua. Kukutana na wananchi
hawa kutatoa nafasi nzuri ya kujadili namna bora ya kuendesha mikakati yote ya kulinda
hifadhi ili kwa kushirikisha wananchi na pia kwa kuzingatia haki za binadamu na utawala
bora.
- b) Zoezi la kuhamisha watu katika eneo hilo la Ngorongoro lisitishwe ili kutoa nafasi ya
kujipanga upya kwa kutoa nafasi kubwa ya wananchi kushirkiishwa na kufanyia kazi
mapendekezo ya wadau mbalimbali wakiwemo watetezi wa haki za binadamu. Watetezi
wa Haki za binadamu waliandaa taarifa mwaka 2023 yenye mapendekezi mengi kuhusu
namna bora ya kuepuka ukiukwaji wa haki za binadamu katika jitihada zinazochukuliwa
za kulinda hifadhi na ikolojia.
- c) Kuacha kutoa vitisho kwa watetezi na waandishi wa habari wanaofuatilia haki za wananchi
katika eno hili. Badala yake wapewe ushirikiano na mamlaka zote zinazohusika na eneo
hili.
- d) Serikali na mamlaka zote ziendelee kuheshimu na kulinda haki za wananchi ambao
hawajaamua kuhama kwa kwenda maeneo mengine.
- e) Jitihada za kuboresha huduma za jamii zifanyike kwa haraka, mfano shule zote zifanyiwe
ukarabati wakati huu ambapo wanafunzi wanafunga shule.
- f) Bajeti iliyotengwa ina onyesha ni ya kufanya ukarabati pekee, tunashauri Tarafa ya
Ngorongoro itengewe fedha kubwa toka serikalini na pia toka kwa NCAA ili kuboresha na
kuongeza miudo mbinu mingine ambayo kwa sasa zinazosekana katika huduma zote za
kijaamii.
- g) Kurejesha huduma ya afya ya dharura kwa njia ya ndege. Huduma hii ilikuwepo na iliweza
kuonesha mafanikio makubwa.
- h) Kurejesha huduma za kifedha katika hospitali ya Enduleni. Kulikua na utaratibu wa serikali
kuwapa Hospitali na Enduleni million 300 za kitanzania kila mwaka.
- i) Kuruhusu wadau wa maendeleo na watetezi wa jamii kusaidia katika kuboresha huduma
za jamii katika tarafa ya Ngorongoro.
- j) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iboreshe na kutenga au kushauri Serikali itenge
budget ya kutosha kwa ajili ya kuboresha huduma ya ada kwa wanafunzi wanaochaguliwa
na Baaraza la Wafugaji Ngorongoro kwa ajili ya huduma hii.
- k) Kuendelea kuboresha uhuru wa wananchi wanaoishi katika Tarafa ya Ngorongoro.
- l) Mkakati wa kuimarisha Baraza la Wafugaji Ngorongoro uanze kwa lengo la kutoa nafasi
ya wananchi kuwa na chombo chao imara.
Imetolewa leo 18/11/2024 na
Wakili Onesmo Olengurumwa,
Mratibu Taifa, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania