Site icon A24TV News

NMB foundation wampatia ufadhili mwanafunzi IAA.

Na Mwandishi wa A24tv Arusha

Mwanafunzi Selesi John Njacha anaesoma chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) amefanikiwa kupata ufadhili wa masomo pamoja na msaada wa vifaa kupitia mpango wa ‘NMB nuru yangu Scholarship and Mentorship’ inayotolewa na Asasi ya Kiraia ya NMB Foundation.

 

Selesi anaesoma Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Usalama wa Mtandao (Cybersecurity) mwaka wa pili amepata ufadhili huo utakaojumuisha malipo yote ya ada, nauli, posho, vifaa vya kusomea na kuandikia(stationary), mafunzo ya vitendo ‘field’ na laptop.

Akibidhi vifaa hivyo vya kujifunzia leo Novemba 13,2024 jijini Arusha, Meneja wa NMB kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kuwa Mwanafunzi huyo atalipiwa malipo yote yatakayolewa na shule kwa miaka yote ya shahada ya kwanza pamoja na vifaa vya kujifunzia.

 

“Ufadhili huu unaotolewa na Asasi ya Kiraia ya ‘NMB Foundation’ iliyo chini ya Benki ya yetu, unatolewa kwa wanafunzi wanaojiunga chuo katika fani za Hesabu na Takwimu, Biashara, Uchumi, Teknolojia, Habari na Mawasiliano, Uhasibu, Uhandisi, Mafuta na Gesi, Sayansi pamoja na Udaktari”amesema Baraka.

 

Amesema kuwa wanatoa ufadhili huo kwa wanafunzi wanaotoka mazingira magumu au familia yenye changamoto lakini wana ufaulu mzuri kwa masomo yao ya kidato cha Sita kwa Daraja la Kwanza pointi 3-7, hivyo kuwataka wahitimu wote wa kidato cha sita wenye sifa hizi wajitokeze kuomba udhamini kwenye tovuti yao au kutembelea matawi ya benki ya NMB kupata maelezo zaidi.

 

“Lengo la ufadhili huu ni kuhakikisha hakuna kijana mwenye kupambania ndoto zake za kielimu anabaki nyuma kwa sababu tu hana uwezo au familia yake ina changamoto yoyote hivyo tunampongeza sana Selesi na tunatarajia atakuwa kielekezo muhimu cha NMB foundation na kuwaelekeza wenzake waombe fursa hii na waitumie” amesema Baraka.

 

Akizungumzia ufadhili huo, Selesi alisema kuwa utamsaidia kufikia ndoto zake za kuja kuwa m’bunifu wa teknolojia hasa katika maswala ulinzi.

 

“Familia yangu ni duni, nilikuwa nasoma hapa kwa michango nikiwa siijui kesho yangu ya kumaliza masomo na kutimiza ndoto zangu kabla ya kuonyeshwa na mwenzangu juu ya program hii ya Nuru yangu, naishukuru benki ya NMB kwa kunihakikishia hatma ya masomo yangu” alisema.

“kwa sasa naweza kuahidi Taifa kuwa linaweza kuja kunitegemea katika ubunifu wa teknolojia itakayosaidia ulinzi wa jamii na nchi yangu, hivyo niombe wenzangu ambao wana juhudi katika elimu, changamoto ya umaskini usiwarudisha nyuma bali wapambanie ndoto zao” amesema.

 

Awali wakati akifungua dirisha la pili wa Ufadhili wa Masomo na Usimamizi mwaka 2023/2024, kwa wanafunzi wanaojiunga Vyuo Vikuu kupitia Programu ya NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna alisema msimu huu mpango huo itafadhili wanachuo 65 kwa kiasi cha Sh. Bilioni 1.0 zilizotengwa.

 

Alisema hadi sasa zaidi ya wanafunzi 130 wanafadhiliwa katika mpango huo na wanaendelea na masomo katika vyuo vikuu mbalimbali na kuwataka wengine wenye sifa kujitokeza kupakua fomu kwenye tovuti ya NMB Foundation na kujaza kwa usahihi ili waweze kunufaika na fursa hiyo na kuwa kielelezo cha mabadiliko ya kielimu nchini.