Site icon A24TV News

NMB wamwaga mamilioni kuhamasisha matumizi ya kibenki .

Na Mwandishi wa A24tv .Arusha .

Katika kuhamasisha utamaduni wa watanzania kujiwekea akiba ili kukabiliana na dharura zinazoweza kujitokeza za uhitaji wa fedha, Benki ya NMB imetoa zawadi kwa wateja wake kupitia kampeni ya ‘Bonge la Mpango, mchongo ndio huu’.

Zawadi hizo zimetokana na washindi wa bahati nasibu inayochezeshwa na benki hiyo kwa wateja wake waliojiwekea akiba ya kuanzia shilingi 100,000 na kuendelea.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Meneja wa NMB kanda ya kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kampeni hiyo ya kila mwaka ya ‘Bonge la Mpango’ inalenga kuhamasisha watu kufungua akaunti na kujiwekea akiba ili kutatua matatizo ya dharura yanayohitaji fedha .

Amesema zawadi wanazotoa kwenye kampeni hiyo ya kila mwaka inayodumu kwa miezi 12 ni pamoja na kitita cha shilingi milioni 100 kila mwaka, 100,000 kila wiki, friji, TV, pikipiki ya magurudumu mawili (Toyo) na pikipiki ya magurudumu matatu (Guta na Bajaji sambamba na mashine ya kufulia,majiko ya Gesi, trekta za kilimo (Power tiller).

“Zawadi hizi tangu kuanzishwa msimu wa nne zimefanikiwa kuhamasisha watu wengi kufungua akaunti na kujiwekea akiba ambazo zimekuwa msaada mkubwa wa kuwaepusha na mikopo umiza wanapopata shida ya tatizo la kifedha” amesema Meneja huyo.

Kwa mwezi huu, washindi watano wamefanikiwa kukabidhiwa zawadi zao akiwemo Issa Bakari Hassan aliyekabidhiwa pikipiki ya magurudumu matatu maarufu kama ‘Guta’ na Shillah Gabriel aliyekabidhiwa TV yenye ukubwa wa nchi 75.

Mbali na hilo, droo nyingine ilichezeshwa papo hapo na washindi watatu kupatikana akiwemo Bernard Kimaro (Kahama) aliyejishindia zawadi ya power tiller, Deogratius Kisoka (Mwanza) aliyezawadiwa pikipiki ya magurudumu mawili (Toyo) na Meshack Mafie aliyezawadiwa simu janja.

Akizungumzia kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Amiri Mkalipa amesema kuwa kampeni hiyo ni muhimu kwa wananchi wote hasa wafanyabiashara ambao wamekuwa na dharura ya kifedha mara kwa mara hivyo kuwataka kuchangamkia fursa hiyo.

Pia aliwataka NMB kutembea mara kwa mara kwa wananchi walioko pembezoni wakiwemo wakulima katika wilaya yake ambao wamekuwa wakipata changamoto za kifedha mara kwa mara lakini kukutana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu na kuwaingiza kwenye mikopo umiza.

Akizungumzia zawadi aliyoshinda, Hassan amesema kuwa Guta hiyo itamsaidia katika usafirishaji wa bidhaa zake za nafaka ambazo amekuwa akitumia gharama kubwa kufikisha katika kituo cha biashara kutokana na kukodisha usafiri.

“Nashukuru sana NMB, kwa sasa nina usafiri wangu sio mchana wala usiku niko huru kuhamisha nafaka zangu katika minada mbalimbali bila kujali gharama, tofauti na mwanzo nilikuwa napoteza zaidi ya 150,000 hadi 200,000 kwa usafiri pekee wa kuzunguka katika minada kufuata wateja na kufanya faida yangu kuwa ndogo” amesema.

‘NMB Bonge la Mpango’ ni msimu wa nne sasa kufanyika inayokwenda na kauli ya fungua Akaunti, Weka Akiba na Ushinde ambapo kwa msimu huu mshindi wa jumla anatarajiwa kutangazwa desemba 19,2024 na kukabidhiwa kitita chake cha shilingi milioni 100 taslimu.

Mbali na hilo kila wiki washindi 10 wanaendelea kujinyakulia kitita cha shilingi 100,000 na vifaa mbalimbali, huku washindi wanne wa kila mwezi wakipewa shilingi milioni tano kila mmoja.

mwisho